Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO limeorodhesha tamasha la Shuwalid la Ethiopia chini ya urithi wa dunia.
Shuwalid ni tamasha la kila mwaka la siku tatu linaloadhimishwa na watu wa Harari wa Ethiopia. Tamasha hilo, linaashiria mwisho wa siku sita za kufunga ili kufidia makosa yaliyoachwa wakati wa Ramadhani.
Uamuzi huo umefanywa na kamati ya kikao cha kumi na nane cha kamati ya kiserikali ya kulinda urithi wa tamaduni zisizogusika kinachofanyika huko Kasane, nchini Botswana kuanzia Jumatatu tarehe 4 hadi Jumamosi tarehe 9, Desemba 2023.
Watu wa Harari husherehekea Shuwalid kwenye madhabahu ya Aw Shulum Ahmed na Aw Akebara, yanayopatikana kwenye lango kuu la kuingilia jiji la Harar.
Tamasha huanza na dua na nyimbo, ikifuatiwa na usomaji wa maandiko, muziki na ngoma.
Sherehe hiyo inahitimishwa kwa maneno ya baraka.
Hafla hii inawaunganisha wanajamii wa kila rika na jinsia na hutumika kama jukwaa kwa wazee wa jamii kushiriki maarifa na uzoefu wao na kutoa baraka kwa vizazi vijavyo, na pia kwa vijana kujifunza juu ya maadili ya kitamaduni, kanuni na mila.
Shuwalid hupitishwa ndani ya familia na kwa watu kushiriki katika sherehe, na pia kupitia hatua rasmi za elimu na ulinzi katika maeneo ambayo tamasha hufanyika.