Filamu za Kituruki zazoa umaarufu Afrika Mashariki

Filamu za Kituruki zazoa umaarufu Afrika Mashariki

Tamthilia za televisheni na sinema zilizotengenezwa Uturuki zimekuwa ni gumzo na hata kupenya katika masuala ya kijamii na kiutamaduni katika bara la Afrika

Ni usiku wa Ijumaa, Mama Amiri ameshamaliza shughuli zake zote kwa wakati na kuhakikisha chakula cha usiku kinakuwa mezani ifikapo saa moja kasorobo. Mume wake, Mohamed, hana kauli kwa wakati huu kwa sababu huu muda mkewe ameshaupangilia tayari.

Tamthilia maarufu ya Kituruki “Our Story” inaoneshwa kwenye runinga na itafuatiwa na mfululizo wa vipindi vyengine vya Kituruki ambavyo vitaendelea mpaka usiku.

Mohamed Siraji, 47, mkazi wa jiji la Arusha, kaskazini mwa Tanzania, ambaye ni baba wa familia, anafahamu fika kwamba hawezi kupambana na familia yake ifikapo saa moja kamili usiku katika siku za wiki na familia yote ikiwa imekaa sebuleni. Iwe ni kuangalia kandanda au taarifa ya habari. Kituo kitabadilishwa baada ya muda fulani.

“Mke wangu anahakikisha amemaliza shughuli zote kabla ya kipindi kinachoanza saa 1 mpaka saa 5 usiku. Na sio yeye pekee, familia nzima inaungana nae. Kwa muda huo nakuwa sina usemi,” anasema Siraji.

Siraji, kama walivyo watanzania wengine wengi, hajui hata neno moja la Kituruki lakini anafurahia kutizama tamthilia ambazo zimetafsiriwa kwa Kiswahili.

“Tunatazama `Revenge` (Intikam), `Our Story` (Bizim Hiakye) na Ottoman,” anaeleza Siraji, na anaongezea kuwa hana tatizo kuziangalia akiwa na familia yake kwa sababu ni tamthilia zenye “elimu na burudani.”

“Kuna tamthilia moja hiyo, inaonesha umuhimu wa imani na maadili mema,” Siraji anaiambia TRT Afrika, akirejea tamthilia ya Ertugrul, moja ya tamthilia maarufu za wapiganaji wa Kituruki wa karne ya 13 na baba wa Osman Ghazi, mwanzilishi wa dola ya Ottoman.

Kwa Tanzania, majina ya tamthilia za Kituruki ambazo zinabamba ni pamoja na ‘Binti wa Balozi,’ `Nge` ambayo kwa Kituruki ni ‘Akrep,’ Sultan, `Moto wa tamaa` kwa kituruki ‘Hayat Sarkisi’, `Mtego wa Mapenzi` kwa Kituruki ‘Afili Ask’, ‘Hercai’ na ‘Mrs Fazilet na binti zake’.

Burudani ya ‘kistaarabu’

Sampiyon

Katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kukua kwa upatikanaji wa mtandao katika maeneo mengi na kuongezeka kwa utiririshaji wa maudhui mtandaoni, kwa kiasi kikubwa. Afrika mashariki kwa kiasi kikubwa wanatizama kazi kutoka Mexico na Korea ya kusini na tamthilia za mtandaoni huku wakiendeleza mapenzi yao na filamu za Kihindi.

Lakini mafanikio makubwa kwa hakika yamefikiwa na filamu za Kituruki kutokana na ufuatiliwaji wake mkubwa, ambapo kwa kiasi kikubwa mazingira ya kiutamaduni, kijamii yanashabihiana na imani ya ukanda huu.

Salma Katima, 25, kutoka Dar es salaam anasema kwamba anapenda filamu za kituruki kwa sababu “Zinakuruhusu kuufahamu utamaduni wao”

“Mhusika wangu pendwa ni Sankar Efeoghu toka kwenye tamthilia ya Ambassador’s Daughter kwa sababu ya kuwa na sifa za uanaume. Ni baba mwenye upendo na kaka na mtoto na wazazi wake pia,” Katima anaiambia TRT Afrika.

Umaarufu wa filamu za Kituruki umefanya idadi kubwa ya mashabiki kuanza kuwafuatilia wahusika wake.

“Napenda simulizi. Napata kuona changamoto zao kama Waislamu, Ndio, nafahamu kwamba ule sio ukweli, ni maigizo. Lakini naona jinsi ambavyo walikuwa wanapambana kueneza Uislamu na kuanzisha taifa.” Anaeleza akirejea tamthilia za kihistoria Payitaht: Abdülhamid, Omar Mohammed kutoka Nairobi, Kenya, anaeleza sababu yake ya kufuatilia tamthilia.

Watoa huduma nao wana nafasi yao

Payitaht Abdulhamid

Azam TV ni moja kati ya chaneli pekee ambayo inarusha filamu za Kituruki nchini Tanzania. Fatma Mohamed ni Mkuu wa Vipindi, na anaelezea ni kwa namna gani tamthilia hizi “zinamfikia kila mmoja.”

“Tuna wateja takribani milioni moja, na idadi kubwa wanaangalia tamthilia za Kituruki, mara nyingi huwa ni jambo la kifamilia. Sio kawaida kukuta watu wakiangalia vipindi vya namna hii huku wakiwa pekee yao.”

“Hizi filamu zinaakisi maisha ya watu kwa sababu zinaegemea zaidi kwenye masuala ya familia na ya kihistoria” anasema Augustine Malusu, Afisa Masoko na Mauzo wa Star Times, Kampuni ya Habari kichina ambayo imekita mizizi, ambapo tamthilia za Kituruki zinaoneshwa kwatika nchi 12 kwa kupitia huduma zao.

“Startimes ilianza kuonesha vipindi vya kituruki mara baada ya kugundua kwa jinsi gani vimekuwa maarufu nchini Tanzania. Kwa upande mwingine hili lilitufanya tubadili baadhi ya ratiba zetu na kuanza kuonyesha tamthilia kama vile "Ambassador's Daughter" (yakituruki) ili kukata kiu ya watazamaji wetu." Malusu akiiambia TRT Afrika.

Vipindi vinafika mbali zaidi ya ukanda wa Afrika Mashariki kwenye nchi za Kenya na Tanzania.

Mogadishu Cable TV ya Somalia hutafsiri tamthilia kwa Kisomali, anaeleza Muhammad Onyango, Afisa Masoko wa kidijitali anayefanya shughuli zake jijini Nairobi akitokea Somalia.

“Nadhani umaarufu wake unatokana na ukweli kwamba, Wasomali wanajinasibisha na Makabila ya Kayi kuwa ni waislamu kama wao. Pamoja na kwamba filamu za Kihindi ni maarufu, baadhi ya maneno ya kihindi yanafanana na ya Kituruki, hivyo inakuwa rahisi kwa wao kuelewa.”

Rahma Nsekele ni mtafsiri kutoka Azam TV na hutafsiri tamthilia za Kituruki. Hufuatilia maigizo mara kwa mara wakati huohuo akizifanyia kazi kutafsiri, jambo analosema linampunguzia changamoto kulifanya.

“Hizi tamthilia ni tofauti, nimewahi kufanya kazi ya kutafsiri vipindi vingine kutoka Hispania na Korea, lakini hizi ni za kipekee. Nilianza kutafsiri Sultan, ambayo iliweka msingi wa filamu za Kituruki ghafla na mimi nikajikuta nimekuwa mfuatiliaji kama vile watazamaji wengine.”

Nsekele anasema kazi si ya kitoto, lakini hana shida kwani yeye ni mpenzi wa lugha na pia ni “nafasi yake ya ajira”.

Nini Kinazungumzwa Mtandaoni?

Muhammad Onyango, alitoa hoja kwamba tunapata kuona mbinu ya kimaadili ya maudhui yanayotolewa kwenye filamu na tamthilia za Kituruki ukilinganisha na maudhui ya kimagharibi ambayo hutoa changamoto kuangalia.

Mtumiaji mwingine, Omar Mohammed ni mpenzi wa tamthilia zilizotafsiriwa kwa kiswahili. Tamthilia za Kituruki zimetafsiriwa katika lugha kadhaa ili kuwafikia wengi zaidi.

TRT Afrika