Na Coletta Wanjohi
Rwanda imepokea vitengo vya uzalishaji vinavyoitwa "BioNtainers" kwa ajili ya utengenezaji wa chanjo kutoka kwa kampuni ya dawa ya Ujerumani, BioNTech.
Hivi ni vyumba visafi ambavyo tayari vimewekwa na suluhisho za utengenezaji. Kiwanda hicho nchini Rwanda kitaweza kutengeneza hadi dozi milioni hamsini za chanjo ya Pfizer-biontech Uviko-19 kila mwaka.
"Haitazalishia Rwanda peke yake," anasema Yvan Butera, waziri wa serikali katika wizara ya Afya nchini Rwanda, "itakengeneza chanjo ya bara zima ."
Biontech ilianza ujenzi wa kituo chake cha chanjo huko Kigali mnamo Juni 2022. Viwanda vingine vya mtengenezaji vitapatikana Senegal na Afrika Kusini.
Nchini Kenya, kampuni ya Marekani ya Moderna imekamilisha makubaliano yake na serikali ya Kenya kujenga kiwanda cha kuzalisha chanjo nchini humo.
Kampuni hiyo inasema uwekezaji wake utazalisha dozi milioni 500 za chanjo kila mwaka.
"Hamu ya kuanzisha na kupanua vituo vya utengenezaji wa chanjo na utengenezaji wa bidhaa za afya katika bara inaongezeka," anasema Dkt. Ahmed Ogwell, kaimu mkurugenzi wa vituo vya Afrika vya kudhibiti magonjwa, Africa CDC. "Tunahimiza mbinu iliyoratibiwa ambapo aina tofauti za chanjo zinatengenezwa na nchi tofauti na viwanda tofauti ili tusiwe na mafuriko ya aina moja ya chanjo," Ogwell anaongeza.
Wito mkubwa barani
Uwezo mdogo wa uzalishaji wa chanjo barani Afrika uliliweka bara hili katika changamoto kubwa wakati wa vipindi vya dharura vya janga la Uviko-19. Nchi zililazimika kutegemea usambazaji wa chanjo kutoka nchi zilizoendelea.
Shirika la Afya duniani, linasema nchi zinazozalisha chanjo ni chahe, mkiwemo Afrika Kusini, Misri, Morocco, Senegal na Tunisia. Inasema ni asilimia moja tu ya chanjo zinazotumiwa katika bara hili zinatengenezwa hapa.
Bara kujitosheleza katika utengenezaji wa chanjo kutoka mwanzo hadi mwisho- hata hivyo, kutachukua muda. Africa CDC inalenga nchi za Afrika kuendeleza, kuzalisha, na kusambaza angalau 60% ya chanjo zake ifikapo mwaka 2040.
"Zaidi ya mipango mpya 30 ya utengenezaji wa chanjo sasa tayari inaendelea barani Afrika, na kasi inaongezeka ili kuwezesha upanuzi huu," anasema Dkt. Ahmed Ogwell, kaimu Mkurugenzi wa Africa CDC.
Utafiti wa Umoja wa Afrika kuhusu utengenezaji wa chanjo unaonyesha kuwa nchi nyingi hazina programu za kutosha za elimu ambazo ni muhimu kwa utengenezaji wa chanjo. Baadhi ya wale ambao wana ujuzi huishia katika nchi nje ya Afrika zenye ambapo malipo ni bora zaidi.
Africa CDC pia inahimiza nchi barani kuangalia mipango ya bidhaa zingine za afya.
"Tunahitaji kutengeneza vifaa vyetu wenyewe vya uchunguzi, matibabu, na hatua za kukabiliana kama vile barakoa na vifaa vya kinga ya kibinafsi," anasema Dkt. Ogwell.
Mswada katika Shirika la Biashara Ulimwenguni wa kuwa na upanuzi wa msamaha wa haki miliki kwenye chanjo za Uviko-19 na vifaa vya uchunguzi na matibabu inaonekaa kutofua dafu.
Wazalishaji wa kimataifa wa dawa kutoka kwa mataifa yaliyoendelea wanadai kuwa upanuzi wowote wa haki miliki utakuwa na "athari mbaya kwa mfumo mzima wa uvumbuzi."
Lakini Umoja wa Afrika inasema bado umedhamiria kuhakikisha kuwa bara linaanza uzalishaji kwa njia yoyote ile, kwa ajili ya kujikimu mapema kabla ya dharura nyingine ya kiafya kutokea.