Angola imepitisha azimio la kuruhusu angalau nchi 98 kuingia bila visa kwa siku 90 katika juhudi za kukuza utalii wa ndani.
Taifa hilo la Kusini mwa Afrika liliorodhesha Ureno, Brazil, Cape Verde, Marekani, Urusi na China kuwa nchi za kigeni zilizopewa kipaumbele.
Rais wa Angola Joao Lourenco ameiagiza wizara ya mashauri ya nchi za kigeni kuwasiliana na nchi zilizonufaika kuhusu kuondolewa kwa visa vya watalii.
Vivutio maarufu vya watalii vya Angola ni pamoja na fukwe za tropiki za Atlantiki, jangwa la Namib Kusini mwa Jangwa la Sahara na mito kadhaa.
Kwa aina zingine za visa kama vile kazi, masomo, matibabu au kibali cha makazi, raia wa kigeni lazima watume maombi kupitia njia rasmi.
Mpango maalum kwa utalii
Muda wa siku 90 wa visa bila malipo nchini Angola umetolewa kwa watu wanaofika nchini humo kwa madhumuni ya utalii pekee.
Mataifa kumi na nne (14) ya Kiafrika yamo kwenye orodha ya wanufaika bila visa. Nazo ni Tanzania, Eswatini, Morocco, Lesotho, Rwanda, Zimbabwe, Equatorial Guinea, Botswana, Madagascar, Malawi, Mauritius, Sychelles, Cape Verde na Algeria.
Asia ina nchi 11 kwenye orodha ya wasio na visa. Nazo ni Israel, Falme za Kiarabu, Japan, Qatar, Saudi Arabia, Korea Kusini, India, Indonesia, Singapore, Timor-Leste na China.
Ulaya ina nchi 35 kwenye orodha. Zinajumuisha Utuurki, Urusi, Ujerumani, Uswidi, Uswizi, Jimbo la Vatikani, Jamhuri ya Cheki, Luxemburg, Hungaria, Uholanzi, Monaco, Ubelgiji, Denmark, Uhispania, Uingereza na Ireland.
Na nchi nyingine nyingi kutoka Ulaya, Caribean, Asia na falme za Kiarabu.