Zaidi ya viongozi 150 wa nchi na serikali, pamoja na mamia ya mawaziri, wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na waandishi wa habari wanakusanyika mjini New York kwa ajili ya mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), unaoanza Jumatatu.
Marais wa nchi tofauti barani Afrika tayari wamewasili kwa ajili ya kuwakilisha nchi zao katika mkutano huo.
Mkutano wa marais wa UN una umuhimu gani?
Baraza Kuu, ambalo pia linajulikana kama UNGA, ndilo jukwaa kuu la wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa kujadili masuala ya kimataifa kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Kila Septemba, viongozi wa ulimwengu na wajumbe hukusanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York ili kuzungumzia masuala muhimu zaidi yanayoigusa dunia.
Viongozi wa nchi wanachama hupokezana kutoa hotuba kwa zamu na hupewa haki ya kujibu inapohitajika. Wanatumia fursa hiyo kuibua mada ambayo wanazingatia kama suala muhimu kwa nchi zao.
Viongozi huombwa kutoa hotuba zao katika muda usiozidi dakika 15, hata hivyo viongozi wa dunia mara nyingi hupitisha muda huo.
Je, ni masuala yapi yatayojadiliwa?
Suala la mabadiliko ya tabia nchi litapewa kipaumbele.
" Uharibifu utokanao na mabadiliko ya hali ya hewa tayari ni mkubwa, na uzalishaji wa gesi chafu duniani unabaki katika viwango vya juu. Ulimwengu unahitaji kupunguza kwa haraka ongezeko la joto duniani hadi digrii 1.5°C juu ya viwango kabla ya viwanda na kuzuia athari mbaya zaidi," taarifa ya UN inayoelezea mkutano huo imesema.
" Ninaitisha mkutano wa kujadili mabadiliko ya hali ya hewa kwa ajili ya serikali, biashara, mamlaka za mitaa na mashirika ya kiraia," katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema.
"Ni wakati wa kuonyesha uongozi unaoaminika na ambao ni madhubuti ya kulinda maisha kutokana na athari za shida ya hali ya hewa," ameongezea.
Afya pia itajadiliwa kwa kina
Bado kuna wasiwasi kwamba kuibuka tena kwa magonjwa yanayoathiriwa na mlipuko kunaendelea huku nchi zikitambua kwamba janga la Uviko-19 bado lina athari kubwa kwa nchi za kipato cha chini.
Viongozi pia watakuwa na kongamano ambapo watajadili magonjwa mengine kama kifua kikuu na ukimwi.
Amani na usalama iko kwenye ajenda
Mkutano unafanyika huku kukiwa na athari kubwa duniani ya vita vya Ukraine na Urusi, ambavyo zimesababisha kuwepo kwa upungufu wa chakula hasa kwa nchi ikiwemo za Afrika ambazo zimekuwa zikinunua chakula kutoka Ukraine.
" Huku Baraza la Usalamala Umoja wa Mataifa likiwa limegawanyika na wanachama wa Umoja wa Mataifa kutokubaliana kuhusu mizozo tofauti," Shirika la International Crisis Group limesema katika ufafanuzi wake wa mkutano wa mwaka huu wa Umoja wa Mataifa.
" Katika kipindi cha 2023, shinikizo linalohusiana na vita vya Urusi na Ukraine limekuwa na athari kwa mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa, ikiwemo Baraza la Usalama," shirika hilo limesema.
" Kama jumuiya ya mataifa iliyojengwa juu ya dhana ya usalama wa pamoja, tunapaswa kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha ushirikishwaji na kwamba sauti zote ziwe kubwa au ndogo, zenye nguvu au vinginevyo zinasikika," Dennis Francis rais wa Trinidad and Tobago.
Mapinduzi ya hivi karibuni ya baadhi ya serikali barani Afrika ikiwemo Gabon, Mali na Niger pia huenda yakafika kwenye jukwa kuu la majadiliano ya dunia.
Trinidad and Tobago ndiye kiongozi wa mkutano wa mwaka huu.