Ndugu, jamaa na marafiki wakishiriki zoezi la kumsitiri mpendwa wao ambaye alikuwa mshiriki wa kanisa lililokuwa linaongozwa na  Paul Mackenzie wa Kenya./Picha:  REUTERS/Amina Denge    

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mnamo Aprili 2023 mwanaume mmoja alikwenda kwenye kituo kimoja cha Polisi nchini Kenya, kutoa ripoti ya kupotelewa mkewe na binti yake.

Mtu huyo alikuwa na nia moja tu; ya kujua alipo mkewe na binti yake ambao walikuwa wamejiunga na kanisa linalomilikiwa na mhubiri Paul Mackenzie, bila kujua kuwa ripoti yake ingefunua ukurasa wa wapi walipo mamia ya watu ambao walikuwa bado wanatafutwa na ndugu zao.

Siku zi nyingi, mamlaka za nchini Kenya zikaja kubaini uwepo wa makaburi ya halaiki walimozikiwa watu zaidi ya 400, katika ardhi yenye ekari 800 ndani ya msitu wa Shakahola, kwenye eneo la pwani ya Kenya.

Hata aliposimama kizimbani, bado mamia ya wafuasi wa Mackenzie walikuwa hawajulikani walipo, ama kama wangali hai au wamekwisha kufa.

Wakati baadhi ya ndugu walibahatika kupata mabaki ya ndugu zao kupitia vipimo vya vinasaba, bado wengine wanaendelea kuhaha kutaka kujua walipo wapendwa wao.

Hata aliposimama kizimbani, bado mamia ya wafuasi wa Mackenzie walikuwa hawajulikani walipo, ama kama wangali hai au wamekwisha kufa./Picha: Reuters

Uwepo wa makaburi hayo katika eneo la msitu wa Shakahola, ni kati ya matukio yaliyoibua hisia za wengi nchini Kenya, huku wachambuzi wa mambo wakinyooshea kidole udhaifu katika sheria.

"Kenya bado haijaridhia mkataba wa kimataifa ulinzi wa watu wote dhidi ya kutoweka na kutekwa kutoweka, hivyo inakuwa ngumu hata kuwatia nguvuni wanaotuhumiwa kwa makosa hayo," anasema Ramadhan Rajab, mwanaharakati mwandamizi kutoka kutoka Shirika la Amnesty International Kenya.

Anaongeza: "Kwa hiyo, si kosa kumtowesha mtu kwa lazima nchini Kenya kwani hakuna hakuna sheria ya kuwajibisha hadi mabaki ya miili yao ipatikane ... , watu wanashitakiwa kwa sheria za utekaji nyara, hii haifai.

Ukiwa umeanza kutumika tarehe 23 Disemba, 2010, sehemu ya Mkataba wa Kimataifa wa kwa Ajili ya Ulinzi wa Watu Wote Waliotekwa na Kuwekwa Vizuini unasema yafuatayo:

"Kila nchi mwanachama itachukua hatua zinazohitajika ili kumwajibisha kisheria mtu yeyote ambaye anatenda, kuamuru, kuomba au kushawishi kutendeka kwa, kujaribu kutenda, ni mshiriki au kushiriki katika kupotea kwa mtu mwingine ".

Kulingana tovuti ya Umoja wa Mataifa, nchi chache za Kiafrika ambazo zimeidhinisha mktaba huu wa kimataifa ni pamoja na Burkina Faso, Côte d'Ivoire, Gabon Gambia, Malawi, Mali, Mauritania, Nigeria, Niger, Senegal, Afrika Kusini, Sudan na Zambia.

Mamlaka za nchini Kenya zilibaini uwepo wa makaburi ya halaiki walimozikwa watu zaidi ya 400, katika ardhi yenye ekari 800 ndani ya msitu wa Shakahola, kwenye eneo la pwani ya Kenya./Picha: TRT Afrika

Nchini Kenya, serikali imekuwa ikinyooshewa vidole kutokana na vitendo vya watu kupotea.

"Bila hofu yoyote ya utata, hakutakuwa tena na mauaji ya watu au mauaji ya kisiasa," Rais William Ruto aliwahi kunukuliwa akisema siku ya Aprili 21, 2024 wakati wa ibada moja kanisani nchini Kenya.

Hata hivyo, miezi mitatu baada ya kauli hiyo, wakenya walipigwa na butwaa kufuatia taarifa za kupatika kwa miili mingine sita ya wanawake, iliyokuwa imefungwa na kutupwa kwenye jalala moja huko Nairobi.

Siku tatu baadaye, Polisi nchini Kenya walimkatama Collina Jumaisi, ambaye alikiri kuhusika na mauaji ya wanawake wengine 42, lakini alikana tuhuma hizo, mara tu baada ya kufikishwa mahakamani.

Mshukiwa huyo, aliripotiwa kutoroka kutoka katika kituo cha Polisi cha Gigiri jijini Nairobi, Agosti 15, 2024, tena akiwa chini ya ulinzi wa polisi, tukio lililoibua maswali mengi.

Washiriki wa Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya na maafisa wa polisi wakimhudumia mshiriki aliyedhoofika wa dhehebu la Kikristo kwa jina la Good News International Church, ambaye waumini wake waliamini kwamba wangeenda mbinguni ikiwa wangejiua kwa njaa, katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi, Kenya Aprili 23. , 2023. REUTERS/Stringer

Matukio ya watu 'kupotea' bado ni tatizo barani Afrika

Nchini Uganda ambapo mkataba huo bado haujaridhiwa, mwanamke mmoja anamlilia mumewe.

Sarah Damulira hajamwona mumewe kwa miaka minne sasa, na analazimika kulea familia yake yenye watoto saba, peke yake

"Tulisikia kwamba alikuwa amekamatwa tangu 2020 na kupelekwa polisi lakini tangu wakati huo nimekuwa nikimtafuta kwenye magereza tofauti bila mafanikio yoyote," Damulira anailezea TRT Afrika.

Hata hivyo, inaaminika kuwa mumewe, aitwaye John alitekwa nyara na vikosi vya usalama mnamo Novemba 2020.

Hii ilikuwa katika kilele cha kampeni za urais nchini Uganda , wakati mwanasiasa ambaye pia ni mwanasiasa maarufu nchini humo Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine alipotaka kumuondoa madarakani Rais Yoweri Museveni.

Familia yake bado inaamini kuwa mpendwa wao alitoweka kutokana na sababu za kisiasa, hatua iliyolaaniwa na kukosolewa na makundi ya kisiasa na haki za binadamu nchini humo.

Ripoti zinaonesha kuwa watu wengine katika maeneo ya bara la Afrika wamelazimika kutoweka kutokana na migogoro ya kivita iliyodumu kwa muda mrefu barani Afrika, majanga ya asili, ambayo baadhi yamechangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Serikali ya nchini imekuwa ikinyooshewa vidole kutokana na vitendo vya watu kupotea./Picha: TRT Afrika

Hali kadhalika, baadhi ya watu haswa kutoka nchi za pembe ya Afrika wamezikimbia nchi zao na kwenda mataifa ya uarabuni kutafuta kile wanachokiita 'maisha bora'.

Kulingana na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), zaidi ya watu 71,000 barani Afrika wanaripotiwa kupotea, ambayo ni asilimia 75 kutoka idadi iliyorekodiwa mwaka 2019.

Nayo Tume ya Afrika ya binadamu na haki za watu (ACHPR) imeungana na mashirika mengine ya kimataifa kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kukomesha janga hili.

"Waathiriwa wa matukio ya kutoweka bado wanakabiliwa na changamoto zisizovumilika...tunafanya upya mshikamano wetu na waathiriwa wa kutoweka kwa nguvu, pamoja na mashirika, watetezi wa haki za binadamu na wanasheria wanaowaunga mkono,” inasema taarifa yao ya pamoja.

Wito wa kimataifa

Kila mwaka Agosti 30, dunia huadhimisha siku ya Kimataifa ya Wahanga wa Matukio ya Kutoweka na Utekaji, ambayo kimsingi huangazia dhuluma kubwa wanayokabiliwa nayo watu wengi na familia zao kote ulimwenguni na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kuzuia ukatili huo katika siku zijazo.

Siku hiyo iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2010, inalenga kuangazia hatma ya watu ambao wametoweka kwa nguvu, mara nyingi na maafisa wa serikali au kwa ushirikiano wa serikali.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa./Picha: Getty

Kwa mwaka huu, mashirika ya haki za binadamu yamezitaka nchi za Kiafika kuhudhuria kongamano la kwanza la Dunia la kujadili swala hili (World Congress on Enforced Disappearances) lililopangwa kufanyika tarehe Januari 15 na 16, 2025 huko Geneva, Uswisi.

Mkutano huo umelenga kuhimiza uidhinishaji wa jumla wa Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi wa Watu Wote dhidi ya Kutoweka na Utekaji.

"Kuidhinishwa kwa mkataba kutazipa nchi zetu nafasi nchi zetu kuunda sheria maalumu ndani ya nchi zao zitashughulikia moja kwa moja wale waliopatikana na hatia kwa makosa ya aina hayo," anasema Rajab.

Anaeleza: Kwa waathirika, haya ni mateso makubwa kwa familia zao kwnai wanaweza kupata msongo wa mawazo na athari zingine za kisaikolojia kwani hawajui walipo wapendwa wao.

Anaonya kuwa kutokuwa na sheria za kushughulikia matendo ya namna hiyo yanaweza kuhatarisha amani na usalam wa nchi yoyote ile.

" Inawafanya watu kutokuwa na imani kwa sheri ya ndani na mahakama na pia wahalifu wanaweza kuchukua fursa ya kuwapoteza wapendwa wao au watu ambao wana ugomvi nao wakijua kuwa hakuna sheria ya kuwahukumu moja kwa moja," Rajab anaongeza.

TRT Afrika