Michuano hii inafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na washindi wanakutana katika fainali jijiji Nairobi/ Picha TRT Afrika

Na Suleiman Jongo

TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania

Tanzania kwa mara ya kwanza itashiriki katika michuano mikubwa ya mchezo wa gofu Afrika Mashariki, NCBA Golf Series itakayofanyika Desemba 1, 2023 jijini Nairobi, Kenya

Shariff Salim na Ayne Magombe watapeperusha bendera ya Tanzania katika michunao hii baada ya kuibuka washindi katika michuano ya NCBA Golf Series, iliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania katika viwanja maarufu vya Dar es Salaam Gymkhana Club.

Hivyo, michuano hii rasmi inakuwa ni ya Afrika ya Mashariki.

Michuano hii inafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na washindi wanakutana katika fainali jijiji Nairobi ambapo zaidi ya wachezaji 200 watashiriki ikiwemo wachezaji wa ridhaa (Amateur) na wakulipwa (Professionals, huku zawadi kubwa ikiwa ni kiasi cha shilingi100,000 za Kenya kwa kila mshindi katika nafasi tatu bora.

Tayari michuano hii imefanyika mara nne nchini Kenya na imekuwa na mafanikio makubwa.

waandaaji wa shindano wanaseama ushiriki wa Tanzania utaongeza ushindani kwa wachezaji gofu wengine wa Kenya na Uganda / Picha : TRT Afrika

Kwa upande wa Uganda, michuano hii imefanyika mara mbili na Tanzania imefanyika kwa mara ya kwanza mwishoni mwa wiki ambapo zaidi ya wachezaji 100 wameshiriki katika michuano hii ya mashimo 18.

Salim Sharrif aliibuka mshindi wa jumla wa baada ya kufikisha pointi 76.

"Ninajisikia furaha sana kuwa mshindi wa michuano hii ya kwanza kufanyika nchini Tanzania,” anasema Salim.

”Ushiriki wangu katika fainali za Nairobi utanipa fursa ya kujulikana zaidi na kutanua wigo wa kushiriki michuano mingine mikubwa barani Afrika,“aliongeza Salim muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi.

Katika kitengo cha jumla cha wanawake, Ayne Magombe alinyakua nafasi ya kwanza kwa alama 81 na kuungana na Sharrif kwa ajili ya wawili hawa kuelekea jijini Nairobi na watagharamiwa kila kitu na waandaaji, ikiwemo tiketi za ndege na malazi kwa ajili ya kuiwakilisha nchi.

wachezaji wa Tanzania wamekuwa wakishiriki katika majukwaa ya mashindano mbalimbali Afrika Mashariki/ Picha TRt Afrika

Waandaaji wa michuano hii wamesema lengo ni kuongeza ushindani na kiwango cha mchezo wa gofu katika nchi za Afrika Mashariki, ili kuwapa fursa wachezaji kwa ajili ya ushindani katika michuano mikubwa kama vile PGA Tour na michuano mengine mikubwa ya gofu barani Ulaya katika miaka kadhaa ijayo.

Gift Shoko, afisa wa NCBA kutoka eneo la ukanda wa Afrika Mashariki amesema ushiriki wa Tanzania utaongeza ushindani kwa wachezaji gofu wengine wa Kenya na Uganda.

Gofu ni mmoja wa michezo inayokuwa kwa kasi nchini Tanzania ambapo wachezaji wa Tanzania wamekuwa wakishiriki katika majukwaa ya mashindano mbalimbali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Katika kitengo cha jumla cha wanawake, Ayne Magombe alinyakua nafasi ya kwanza kwa alama 81/ Picha TRT Afrika

Kuna zaidi ya viwanja 13 vya gofu nchini Tanzania kama vile Dar es Salaam Gymkhana Club, Lugalo, Arusha Gymkhana, Morogoro Golf Club, Mufindi Golf Club, Moshi Golf Club na Kilimanjaro Golf and Wildlife Estate ambapo michuano mbalimbali ikiwemo ya kimataifa hufanyika na wachezaji kutoka nchi za jirani kushiriki.

TRT Afrika