Suleiman Jongo
Nchi za Afrika ya Mashariki, Kenya, Uganda na Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia zinatafuta nafasi ya kuandaa kwa pamoja Fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) za mwaka 2027.
''Matarajio ni makubwa kwa kuwa hivi sasa ni zamu ya Afrika ya Mashariki,'' waziri wa michezo wa Tanzania Daktari Damas Ndumbaro alisema. 'Ni imani ya mataifa haya kukubaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ombi la pamoja la kuandaa fainali hizi.
Dkt Ndumbaro alisema haya baada ya maafisa wa CAF kufanya ukaguzi wa miundombinu, ikiwemo viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Mashirikisho ya soka ya nchi hizi tatu kwa kushirikiana na makatibu wakuu na mawaziri wa wizara za michezo kutoka nchi husika wamekaa mguu sawa kuona jambo hili linafanikiwa baada ya kuweka ushawishi wa kutosha wa kidiplomasia.
Kenya, Uganda na Tanzania kwa pamoja zimetengeneza kauli mbiu inayojulikana kama ’ East African Pamoja Bid’ yenye lengo la kuweka ushawishi katika ombi hilo kwa pamoja, bila shaka yoyote mataifa haya yanaweza kuandaa michuano hii.
Mataifa mengine yaliyowasilisha ombi lao kuwa wenyeji wa AFCON 2027 ni Botswana, Senegal na Misri.
Algeria ilitangaza kujiondoa kutoka kuwania uandaaji wa kombe hilo la ubingwa wa Afrika 2027, Jumanne, siku moja kabla ya kutolewa tangazo hilo na CAF.
Rais mpya wa shirikisho la soka Algeria, Walid Sadi alitangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa wamechukua uamuzi huo ili kuzingatia mkakati mpya wa ukuzaji wa soka nchini Algeria.
Misri tayari imetoka kuandaa fainali za AFCON 2019 na Algeria pia imetoka kuandaa mashindano ya wanawake ya AFCON ya wachezaji wanaocheza ligi ya ndani ya Afrika (CHAN 2023) yaliyofanyika mapema mwaka huu.
Kwa hiyo ina maana kuna uwezekano mkubwa pia Afrika Mashariki ikapata fursa ya 2027. Lakini Je CAF itaweza kuwapa kura hiyo?
Mustafa Juma Abdallah ni mmoja wa mashabiki damu wa kandanda jijini Dar es Salaam, ambaye anasema nchi hizi tatu zina kila sababu ya kuwa mwenyeji.
“Kikubwa zaidi ni uwepo wa mashabiki wenye mapenzi ya mpira wa miguu na Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa mashabiki wanaopenda kandanda kuliko nchi nyingi Afrika, zikiwemo hata zile ambazo ziliwahi kuandaa michuano hii,“ anasema Abdallah.
Abdallah anaungana na mashabiki wengine nchini Tanzania ambao wanasema maandalizi yanayoendelea kufanyika katika nchi hizi ili kukidhi matakwa ya CAF yanaridhisha na kuna kila sababu ya Jumuiya hii kupewa michuano hii ili kuleta soka la Afrika ndani ya Afrika ya Mashariki.
Mashabiki wengi wa kandanda kutoka nchi mbalimbali wataweza kusafiri kwa njia mbalimbali na kufika Afrika ya Mashariki kushuhudia michuano hii.
Kwa mfano, Tanzania pekee inapakana na nchi nyingine 8 katika ukanda huu ambapo mashabiki wanaweza kusafiri hata kwa magari kwa ajili ya kuangalia michuano hii.
”Tupo tayari kuwaona wachezaji wakubwa wa Afrika wanaopiga kabumbu barani Ulaya kuja Afrika na kuona uzuri wa nchi hizi na ukarimu wa watu wake,“ anasema Frank John, shabiki asiyekosekana uwanjani kila mechi kubwa zinapochezwa zikiwemo za kimataifa.
Wakati mashabiki wakiwa na shauku ya kusikia jambo hili linafanikiwa, Mawaziri, akiwemo Daktari Ndumbaro wa Tanzania na viongozi mbalimbali wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) pamoja na wengine wa nchi husika tayari wamewasili Cairo kwa ajili ya kuweka ushawishi wa mwisho kuelekea uamuzi wa kihistoria.
“Kikubwa tayari CAF wameangalia miundombinu kinachosubiriwa ni wao kuamua tu, cha msingi sisi tupo tayari," amenukuliwa Waziri Ndumbaro akisema.
Marais wa nchi hizi, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda na William Ruto wa Kenya wao pia wamejipanga kuhakikisha historia inaandikwa.
Katika kuhakikisha hili linafanikiwa, kila nchi imefanya jitihada kuhakikisha safari hii inakuwa ya mafanikio.
kwa upande wa Tanzania, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha shilingi bilioni 31 za nchi hiyo kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao hivi sasa una uwezo wa kuchukua watu 60,000 wakiwa wamekaa.
Uwanja wa Mkapa kwa sasa ndiyo unatambulika kama miongoni mwa viwanja bora katika ukanda huu wa Afrika na moja ya sababu ya ukarabati wake ni katika utekelezaji wa maagizo ya CAF kwa ajili ya michuano ya kwanza Afrika ya Super Cup, ambayo mabingwa wa zamani Simba na vigogo wengine barani Afrika watautumia kwa ajili ya michuano hiyo.
Rais Samia pia alitangaza ujenzi wa viwanja vingine viwili vipya ambavyo vitajengwa katika mikoa ya Dodoma na Arusha, kila kimoja kikiwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000.
Uamuzi mwengine unaotarajiwa Jumatano hii ni nani atakayeandaa kombe hilo la Afcon 2025.
Baada ya kujiondoa kwa Algeria kuwania kuandaa makombe yote mawili 2025/27, sasa kombe la 2025 limeachiwa kushindaniwa kati ya Morocco, Zambia na ombi la pamoja la Nigeria na Benin.
Shindano hilo la Afcon hufanyika kila baada ya miaka miwili ambapo timu 16 zitapambana nchini Cote d 'Ivore Januari mwakani kwa awamu ya 2023.
Mabingwa watetezi wa Afcon sasa ni Senegal.