Tanzania: Simba, Yanga waanza safari ya mzunguko wa pili wa mechi za awali kufuzu CAF

Tanzania: Simba, Yanga waanza safari ya mzunguko wa pili wa mechi za awali kufuzu CAF

Yanga itamenyana na Al-Merrikh ya Sudan huku Simba ikichuana na Power Dynamos ya Zambia
Mzunguko wa pili wa mechi za awali kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa ya CAF 'CAF Champions League' umeanza. picha: CAF

Vigogo wa soka Tanzania - Young Africans na Simba SC waanza safari ugenini wakiwa mbali na nyumbani katika ngarambe za raundi ya kwanza.

Mzunguko wa pili wa mechi za awali kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa ya CAF umeanza huku vilabu vinajiandaa kujinyakulia tiketi za kushiriki hatua ya makundi ya mashindano hayo maarufu ya klabu bingwa barani Afrika, CAF.

Klabu ya Simba imewasili Zambia kukabiliana na Power Dynamos katika uwanja wa Levy Mwanawasa leo alasiri huku wapinzani wao Young Africans, ambao walimaliza wa pili kwenye Kombe la Shirikisho la CAF TotalEnergies msimu uliopita, wakisafiri hadi Kigali Rwanda kumenyana na Al-Merrikh ya Sudan.

Simba SC wanalenga kujizolea ushindi mara nyingine dhidi ya Power Dynamos. Picha: SImba SC Facebook

Simba iliifunga Power Dynamos 2-0 mara ya mwisho timu hizo zilipokutana mechi ya Kirafiki kwenye Simba Day huku magoli ya Simba SC yalifungwa na Onana na Fabrice Ngoma.

"Tumejiandaa vizuri, na timu tumeiandaa vizuri. Mtamuona Simba halisi ambaye yuko tayari kutawala soka la Afrika. Simba mtakayoiona leo sio Simba ile iliyocheza mechi ya kirafiki," alisema mwenyekiti wa bodi ya klabu ya Simba Salim Muhene kutoka kambi ya timu hiyo mjini Ndola, Zambia.

Timu zote za Yanga na Simba zitakuwa zinawategemea baadhi ya mashabiki wake walioandamana nao kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kwenye msafara wa mabasi hadi Rwanda na Zambia ili kuzipiga jeki timu hizo kwa kuzishangilia uwanjani.

Nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto hajasafiri na timu hiyo. Picha: Yanga FC facebook.

Kwa upande mwingine, Kocha wa klabu ya Yanga Miguel Gamondi ambaye amezungumza kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika amesema kuwa wanatarajia kuondoka Rwanda na matokeo bora na wamejitahidi ipasavyo.

"Ingawa hatujui mengi zaidi kuhusu Al-Merrikh ya Sudan, tunajiamini na tuko na matumaini mazuri." Gamondi alisema.

Aidha ameongeza kuwa, ingawa wamempoteza Nahodha Bakari Mwamnyeto, kikosi chake kiko na wachezaji wa kutosha kujaza pengo lake. " Bakari ni mchezaji muhimu na tuko naye katika kipindi hiki kigumu na tunamtakia mazuri," Gamondi alisema.

Timu za hizi kutoka Tanzania zitakuwa na nafasi bora za kufuzu kwa hatua za makundi ya Ligi ya Mabingwa ya CAF kwani watakuwa nyumbani tarehe 30 Septemba na 1 Oktoba kwenye mechi za mkondo wa pili.

TRT Afrika