Roberto Oliveira Goncalves Do Carmo (Robertinho). Picha: Simba
Klabu ya ligi kuu ya soka nchini Tanzania, Simba SC, imemtimua kocha wake Roberto Oliveira Goncalves Do Carmo (Robetinho).

Kuachishwa kwa kocha huyo kunajiri baada ya debi ya kariakoo kukamilika kwa ushindi wa Yanga wa magoli matano dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

"Klabu ya Simba imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba na Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza Roberto Oliveira Goncalves Do Carmo (Robetinho)." Taarifa ilisema.

Aidha, wekundu hao wa msimbazi wamemtimua kocha wao wa viungo, Corneille Hategekimana.

"Vilevile tumefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wa kocha wa viungo Corneille Hategekimana." Klabu hiyo iliongeza.

Robertinho alitua Simba kutoka Vipers SC ya Uganda maarufu Venoms, na kutia saini mkataba wa miaka miwili mnamo Januari 3, 2023, ikiwa ni katikati ya msimu na kufanikiwa kuiongoza timu ikiwa imesalia na mechi 11 za ligi.

"Uongozi wa Klabu ya Simba unawashukuru Makocha hawa kwa mchango wao ndani ya klabu yetu na inawatakia kila la heri katika majukumu yao mapya." Simba ilisema.

Simba

Robertinho aliiongoza timu hiyo kwenye kambi yake ya mazoezi nchini Uturuki, ambapo iliweza kupiga mechi mbalimbali za kirafiki ilipokuwa nchini Uturuki ikicheza dhidi ya Turan PFK ya Ligi Kuu ya Azerbaijan, Adana na Eyupspor, Zira FC, na Batman Petrolspor A.S.

"Katika kipindi cha mpito kikosi chetu kitakuwa chini ya Kocha Daniel Cadena akisaidiwa na Seleman Matola. Tayari mchakato wa kutafuta makocha wapya umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde." Ilisema barua hiyo iliyotolewa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Simba Sports Club, Imani J. Kajula.

Kocha huyo aliisaidia Simba kufika robo fainali ligi ya mabingwa Afrika ingawa ilipoteza dhidi ya Wydad Casablanca, ligi ya mabingwa Afrika, CAF 4-3 kupitia njia ya penalti.

Robertinho ni kocha wa tano kufukuzwa kwenye ligi kuu ya soka NBC Tanzania baada ya Zuberi Katwila kutemwa na Habefu, Habib Kondo kufutwa na Mtibwa, Cedric Kaze kutengana na Namungo huku Mwinyi Zahera akihama Coastal Union.

TRT Afrika