Michuano ya CECAFA inatarajiwa kufanyika kutoka Julai 20 hadi Agosti 4, 2024, jijini Dar es Salaam, baada ya kutofanyika kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mashindano hayo, ambayo hutumika kama kipindi cha maandalizi ya msimu mpya wa ligi kwa timu za ukanda wa Afrika Mashariki, yalisimama kwa miaka mitatu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukata wa kuyaendesha.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA John Auka Gecheo amesisitiza umuhimu wa mashindano hayo maarufu Afrika Mashariki, katika kuziandaa timu za ukanda huo kwa michuano ya msimu ujao.
“Tunafuraha kuona mashindano haya yakirejea kuandaa timu zetu kwa ajili ya michuano ya Liga ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho na ligi nyengine za ndani," amesema Gecheo.
Wakati washiriki wa michuano hii huwa ni maalamu kwa timu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, Gecheo amebainisha kuwa mwaka huu kuna timu ngeni ambazo sio wanachama zitashiriki michuano ya Kagame Cup 2024 ili kuongeza mvuto na ushindani.
Kulingana na Gecheo, mashindano ya mwaka huu, yatashuhudia ongezeko la timu bingwa kutoka kila nchi 12 wanachama wa CECAFA, ikiwemo Zanzibar.
Timu ya Simba, kutoka Tanzania ndiyo yenye kushikilia rekodi ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingi zaidi, ikiwa imeshinda taji la CECAFA Kagame, mara sita.
Inafuatiwa kwa ukaribu na Yanga pia ya Tanzania, Tusker ya Kenya, ambao wameshinda mashindano hayo mara tano.
Washindi wengine ni APR ya Rwanda, Al Merriekh (Sudan), SC Villa (Uganda), na Gor Mahia iliyotwaa taji hilo, mara tatu.