Na Yusuph Dayo
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu, ameahidi tuzo ya shilingi 20M za Tanzania kwa klabu ya Yanga, kwa kila goli la ushindi wakati wa fainali ya kombe la shirikisho.
Katika hotuba mjini Dar es Salaam, Rais Samia pia aliahidi kutoa ndege itakayowapeleka wachezaji wa Yanga nchini Algeria kwa mechi ya marudio dhidi ya wenyeji USMA baada ya mechi ya kwanza itakayofanyika mjini Dar.
Hii ni kuambatana na mabadiliko yaliyo fanyika katika kanuni za fainali hizo, ambapo umerejeshwa mfumo wa fainali ya 'nyumbani na ugenini' katika kombe hilo la shirikisho.
Rais Samia amekuwa akitoa tuzo kwa vilabu vya Simba na Yanga kwa kila goli katika mechi zao zote za shindano hili, iliyofahamika sasa kama' Goli la Mama'.
Awali Yanga ilitajwa kuwa katika 'fomu nzuri' kupambana na Union Sportive de la Médina, ya Algeria (USMA) watakapo kutana katika fainali ya kombe la shirikisho.
Rais wa klabu hiyo Mhandisi Hersi Ally Saidi amesema kuwa wamejiandaa kukutana na yeyote na ana imani watapata ushindi.
''Ukitazama mechi tulizocheza kufikia sasa, ni wazi kuwa tupo katika hali nzuri, na maandalizi ni ya hali ya juu. Japo najua tuna mechi muhimu zinazotukabili, kwa uwezo wa Mungu tutafanikiwa,'' Amesema Hersi.
Akizungumza na TRT Afrika Alhamis, Hersi amesema kuwa sasa wanajiandaa kwa mechi ya robo fainali ya Azam Federations Cup dhidi ya Singida Mei 21.
Jumatano, Yanga waliwalaza Marumo Gallants, katika nusu fainali ilyojaa mikeke nchini Afrika Kusini na kujitengea nafasi katika fainali dhidi ya USMA ya Algeria.
USMA walikuwa wa kwanza kuingia fainali baada ya kuwacharaza wapinzani wao Asec Mimosa kutoka Ivory Coast 2-0 katika nusu fainali iliyochezwa awali.
Yanga watawapokea USMA nyumbani Dar es Salaam kwa mechi ya kwanza ya fainali, 28 Mei kabla ya kuelekea ugenini Algeria wiki moja baadaye.
Tangu habari za ushindi wa Yanga Jumatano usiku klabu hiyo ime miminiwa sifa kutoka wakubwa na wadogo, wenyeji na wageni.
Ni dhima kuu kwa nchi ya Tanzania kwa kuwa imesubiri miaka 30 kabla ya wachezaji wake kutajwa katika uwanja wa fainali za kombe la shirikisho CAF, ambapo waliowatangulia, ni watani wao wa jadi Simba FC, 1993.
Ushindi wao Yanga unatazamiwa kuwa ushindi kwa Afrika Mashariki kwa jumla kwani ni muda eneo hilo limepata kuwakilishwa katika fainali za mashindano ya vilabu katika bara.