Charles M'mombwa, kiungo wa kati anayesakata soka ya kulipwa nchini Australia, alifunga bao pekee mechini dakika ya 56 na kuipa Tanzania ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Niger kwenye mechi yake ya kwanza ya kufuzu Kombe la dunia FIFA 2026 siku ya Jumamosi.
Bao hilo na ushindi huo Marrakech nchini Morocco, umeifanya 'Taifa Stars' kuwa timu ya kipekee ya Afrika Mashariki, CECAFA, kufungua safari ya kufuzu Kombe la dunia FIFA 2026 kwa ukanda wa Afrika kwa ushindi na pointi tatu muhimu.
Hii imeiwezesha Tanzania kushikilia nafasi ya pili Kundi E kufuatia matokeo ya mechi hiyo Jumamosi ikiwa na pointi tatu muhimu.
Chipolopolo wa Zambia ndio viongozi wa kundi hilo kwa idadi nyingi ya mabao kufuatia ushindi wao wa 4-2 dhidi ya Congo.
Aidha, timu ya Tanzania ilisafiri na kufunga safari ya kurudi Tanzania kupitia ndege ya Airbus A220-300 ya Air Tanzania kwa hisani ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Taifa Stars itachuana Jumanne na Timu ya taifa ya Morocco ambayo tayari imetua Tanzania na kuanza mazoezi kambini.
Majirani Uganda Cranes, walipoteza 2-1 dhidi ya Guinea katika mechi yake ya ufunguzi ya kufuzu kombe la dunia 2026 iliyopepetwa ugani Stade du Municipal huko Berkane, Morocco.
Mechi hiyo ilikuwa ni ya kwanza kwa kocha mpya Paul Put Joseph ambaye aliajiriwa hivi karibuni kwa mkataba wa miaka miwili.
Uganda Cranes iko katika kundi G pamoja na Algeria, Somalia, Guinea, Botswana na Msumbiji.
Aidha, Uganda itashuka dimbani Jumanne kumenyana na Somalia katika mechi yao pili kwenye kampeni ya kufuzu kwa kombe la dunia la FIFA 2026.
Wakati huo huo, Harambee Stars ya Kenya nayo ilianza safari yake ya kusaka tiketi ya kutua Kombe la Dunia 2026 kwa kupoteza 2-1 katika mechi yake dhidi ya Gabon.
Mechi hiyo ilichezwa Alhamisi Novemba 16, 2023, ugani Stade de Franceville nchini humo.
Harambee Stars ya Kenya nayo itaendelea na safari yake Kundi F, kwa kucheza Jumatatu Novemba 20, 2023 dhidi ya Seychelles katika uwanja wa Felix Houphouet Boigny, Abidjan.