Timu ya taifa ya Gambia, ikiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka nchini humo Lamine Kabba Bajo imechangia damu kuwasaidia waathiriwa wa tetemeko la ardhi nchini Morocco.
Mwanzoni kulikuwa na wasiwasi juu ya kuendelea kwa mechi hiyo kutokana na habari za tetemeko la Ijumaa, lakini hatimaye mechi iliendelea kama ilivyopangwa.
''Leo tumetoa mchango wa damu katika kituo cha damu cha Marrakech, kufuatia tetemeko lililosababisha maafa makubwa,'' alisema Rais wa Shirikisho Lamin Kabba.
''Watu wengi wamefariki na wengi zaidi wamejeruhiwa, wakiwa katika hali mahututi,'' ameongezea Lamin.
Baadhi ya wachezaji hao wa timu ya 'The Scorpions' walichangia fedha pia.
''Wachezaji ambao walikuwa na haraka kwenda uwanja wa ndege walitoa mchango wa pesa ili wawahi uwanja wa ndege mapema,'' amesema Lamin.
Scorpions ambao wameshafika nyumbani Jumanne, waliibuka kidedea baada ya kufuzu Kombe la Taifa Bingwa Afrika Afcon, kwa kutoka sare ya 2-2 na Congo Brazaville.
Gambia walipambana kutoka kwa mabao mawili chini zikiwa zimesalia takriban dakika kumi kukatika muda wa kawaida na wakajikomboa katika muda wa mwisho na kujipatia nafasi katika fainali hizo za ubingwa wa Afrika nchini Ivory Coast Januari mwakani.