Rais wa FIFA Gianni Infantino akihutubia Mkutano wa Michezo kwa Maendeleo Endelevu kabla ya michezo ya Olimpiki ya Paris, kwenye ukumbi wa Carrousel du Louvre jijini Paris, Ufaransa, Julai 25, 2024. / Picha: Reuters

Na

Leyla Hamed

Mapema mwezi huu, FIFA ilipaswa kufanya mkutano wa kuamua iwapo Israeli inapaswa kufungiwa kushiriki mashindano ya kimataifa ya soka kwa uhalifu wake wa kivita na ukiukaji wa kanuni na sheria za shirika hilo.

Lakini kwa njia ya uoga, iliahirisha uamuzi huo hadi baada ya michezo ya Olimpiki, ikilinda Israeli na uwajibikaji.

Mwezi Aprili, Chama cha Soka cha Palestina (PFA) kilitoa wito kwa FIFA kuiwekea vikwazo na kukitenga Chama cha Soka cha Israeli kushiriki katika michezo ya FIFA kwa misingi ya haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Badala yake bodi inayosimamia soka iliamua kuchelewesha uamuzi wake uliotarajiwa kutoka Julai, licha ya bodi hio kuamua kesi inayofanana na hio hapo mbeleni ya kuizuia Urusi kushiriki katika michezo ya FIFA ndani ya wiki kadhaa baada ya kuishambulia Ukraine.

Katika taarifa yake, FIFA ilisema "kufuatia maombi ya kuongezwa muda kutoka kwa pande zote mbili ili kuwasilisha kesi zao, maombi yaliokubaliwa na FIFA, muda zaidi unahitajika ili kuhitimisha mchakato huu kwa uangalifu unaostahili."

Sasa itashughulikia suala hilo mwishoni mwa Agosti.

Lakini, kulingana na watu walio karibu na kufuatilia suala hilo, ripoti kutoka kwa wataalamu wa sheria wa FIFA tayari iliwasilishwa kwa chombo hicho wiki moja kabla ya tangazo hili.

Kwa hali yoyote, uamuzi huu haujashangaza.

Kwanza PFA iliwasilisha hadharani pendekezo lake la kusimamisha Israeli kushiriki Kongamano la FIFA lililofanyika Mei huko Bangkok, huku FIFA ikiagiza kufanyika tathmini ya haraka ya kisheria.

Kisha badala ya kuruhusu wanachama 211 wake kupiga kura kwa uhuru kama ilivyo kawaida, FIFA ilipitisha uamuzi huo kwa baraza lake. Baraza hilo lina wanachama 37 wanaoaminiwa na rais wa FIFA Gianni Infantino, gavana wa soka wa Italia na Uswizi, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, na anajulikana kuipendelea Israeli.

Matamshi ya chuki

Uamuzi wa FIFA wa kuahirisha kutoa uamuzi wowote, sasa unafungua njia kwa timu ya taifa ya kandanda ya Israel kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

Jambo la kutisha hapa ni kwamba wachezaji wa kandanda katika kikosi cha taifa cha Israeli wote pia ni askari wa IDF. Huduma ya jeshi ni lazima kwa vijana wa miaka 18, na wale ambao wamefaulu kukwepa kuandikishwa hawaruhusiwi kujiunga na timu ya taifa ya kandanda.

Wachezaji wengi wanaochezea timu ya soka ya Israeli bado wanahudumu katika jeshi, jeshi linalokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, ambalo kwa sasa linashiriki katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu huko Gaza.

Baadhi ya mashabiki wanasema wanasoka hawa "hawafai kulaumiwa kwa maamuzi yao ya serikali," lakini sivyo ilivyo. Wengi mara kwa mara huendeleza jeshi la Israeli na kuchochea mauaji ya halaiki kupitia mitandao yao ya kijamii kwa uwazi.

Kwa mfano, mnamo Novemba, Shon Weissman, mwanajeshi wa zamani wa Jeshi la Anga la Israeli na pia mchezaji wa kandanda wa kilabu ya Italia Salernitana, na timu ya taifa ya Israeli, aliandika kwenye X: "Ni sababu gani ya kimantiki kwa nini tani 200 za mabomu hazijarushwa hadi sasa Gaza?" na akajibu, "Haribu. Bana. Vyoga. Ili kulipiza kisasi cha Mungu."

Wakati huo huo mchezaji mwenzake, Tomer Yosefi kutoka Hapoel Haifa FC katika ligi ya Israeli, alisema: "Safari hii tutaifuta Gaza kabisa."

Hamu ya umwagaji damu haujaonyeshwa tu na timu ya mpira wa miguu ya wanaume. Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya wanawake ya Israeli pia wamepatikana wakichapisha mara kwa mara video zenye picha zao wakiwa wamevalia shati la soka kabla ya kubadili sare zao za jeshi la Israel.

Mifano hii ya uchochezi na kutukuzwa kwa wanajeshi wa Israeli na wachezaji wa Israeli imepita bila kuadhibiwa na Chama cha Soka cha Israeli (IFA). Hii ni pamoja na ukweli kwamba IFA inazingatia kanuni za nidhamu za FIFA, kifungu cha 53 ambacho kinakataza kuchochea chuki na vurugu.

Hata hivyo wanariadha kutoka Urusi na Belarus wamelazimika kufuata sheria kama "wanariadha wasioegemea upande wowote," kushiriki katika mashindano bila bendera, nembo au nyimbo za taifa.

Zaidi ya hayo, Kifungu cha 4(1) cha sheria ya FIFA kinakataza vikali "ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya nchi, mtu binafsi au kikundi cha watu kwa sababu ya ubaguzi, ubaguzi wa rangi ya ngozi, kabila, taifa au asili ya kijamii... ni marufuku kabisa, adhabu yake ni kusimamishwa kwa muda au kufukuzwa."

IFA imeshindwa kuheshimu hili, kama inavyoonekana kupitia mwenendo wa klabu ya soka ya Israeli kutoka Jerusalem, Beitar Jerusalem FC, pia mwanachama wa Ligi Kuu ya Israeli.

Mashabiki wake huimba kwa fahari jinsi walivyo "timu ya kibaguzi zaidi" katika Israeli na mara nyingi hupiga kelele za maneno, kama vile "magaidi," kwa Waarabu wanaochezea vikosi pinzani.

Vilabu vya kandanda vya Israeli pia vinawazuia wazi Waarabu kujiunga na safu yake, na unyanyasaji mkali dhidi ya wachezaji wa Kiarabu unashughulikiwa tu kwa hatua za kinidhamu.

Kutumia michezo kuhalalisha ukalijai wa mabavu

Hata kabla ya Oktoba 7, FIFA ilikuwa na sababu za wazi za kufukuza Chama cha Soka cha Israeli.

Kifungu cha 72 (1) cha kanuni za FIFA kinasema, "vyama vya wanachama na vilabu vyao haviruhusiwi kucheza kwenye eneo la chama kingine bila idhini ya chama hicho."

FIFA imekuwa ikifahamu kuwa IFA imekuwa ikikiuka sheria za FIFA tangu angalau 2013, kwa kuruhusu timu za Israeli kucheza mechi katika makazi haramu kulingana na sheria za kimataifa.

Angalau vilabu vitano vya makazi haramu viko kwenye ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu: Kyriat Arba, Givat Zeev, Ariel, Bikat Hayarden na Ma'aleh Adumim.

Infantino, mkuu wa shirikisho la soka duniani, amepuuza kabisa suala hili, ingawa ni muhimu kwa siasa za kikanda na michezo.

FIFA ina jukumu la kuhakikisha kuwa shughuli zake hazinufaiki kutokana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu. Kwa kufadhili michezo kwenye ardhi ambayo imenyakuliwa kinyume cha sheria kutoka kwa Wapalestina na kuandaa mechi chini ya masharti ya ubaguzi, FIFA inakiuka kanuni zake yenyewe.

Mauaji ya kimbari Gaza

Huko Gaza, ukiukwaji wa haki za binadamu wa Israeli unafikia kiwango kipya cha ukatili. Tangu Oktoba 7, zaidi ya Wapalestina 41,000, wakiwemo watoto 16,000 wameuawa na majeshi ya Israeli. Zaidi ya watu 89,000 wamejeruhiwa huku takriban 10,000 wakiwa bado wamefukiwa chini ya vifusi.

Michezo ya Wapalestina haijasalimika kutokana na ushari wa Israeli unaoendelea.

Katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, viwanja vyote 41 vya soka vya Gaza vimeharibiwa, kuharibiwa kiasi au kugeuzwa kuwa kambi za wakimbizi, vizuizi au makaburi ya halaiki. Mnamo Desemba 2023, picha ziliibuka zikionyesha wanajeshi wa Israeli wakigeuza uwanja wa Yarmouk kuwa kambi ya mateso ambapo makumi ya wanaume, wanawake na watoto walivuliwa nguo zao za ndani na kufumba macho, huku wanajeshi wenye silaha na vifaru wakizunguka uwanja huo.

Kwa mujibu wa PFA takriban 400 ya wachezaji wao wameuawa tangu Oktoba 7, ikiwa ni pamoja na wachezaji wa soka 243, 65 kati yao wakiwa watoto.

Hawa ni pamoja na Nazir al-Nashnash, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 20 ambaye alichezea klabu ya Kandanda ya Bureij Services na Hani Al-Masdar, mwanasoka wa zamani na kocha wa timu ya soka ya Olimpiki ya Palestina.

Unaikumbuka Afrika Kusini? Mfumo wa ubaguzi wa rangi ulikuwa dhahiri sana, walipigwa marufuku ya miaka 30 na FIFA, ambayo ilichukua nafasi muhimu kuhakikisha kuuvunja mfumo huo.

Kigezo kilianzishwa hapo. Kama vile FIFA ilijibu kwa kupiga marufuku haraka kwa Urusi siku nne tu baada ya uvamizi wake wa Ukraine.

FIFA iko chini ya shinikizo kubwa juu ya kutokuwa tayari kuchukua uamuzi ambao tayari umechelewa. Je, hii inaeleza nini kutokuwa na msimamo thabiti na ubaguzi wa kuchukua hatua zaa kimaadili, linapokuja suala la kupiga marufuku Israeli?

Mwandishi: Leyla Hamed ni mzaliwa wa Uhispania mwenye asili yake ya Morocco ni mwandishi wa habari wa soka na mtaalamu wa sheria za michezo anayeishi Uingereza. Kwa sasa anafanya kazi kama mhariri, mwandishi na mzungumzaji wa The Athletic, anayeangazia Ligi Kuu ya Uingereza.

TRT Afrika