Rais wa klabu ya daraja la juu ya Uturuki MKE Ankaragucu, Faruk Koca, akimshambulia kimwili mwamuzi Halil Umut Meler baada ya timu yake kutoka sare dhidi ya Caykur Rizespor. / Picha: AA

Rais wa klabu ya soka ya Kituruki MKE Ankaragucu, Faruk Koca, amewekwa kizuizini kwa kumpiga ngumi mwamuzi Halil Umut Meler usoni baada ya mechi ya ligi, waziri wa sheria wa nchi hiyo alisema.

Yılmaz Tunc alisema siku ya Jumanne kwenye X kwamba watuhumiwa watatu, wakiwemo Koca, walizuiliwa na mahakama ya Ankara baada ya kutoa maelezo yao kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Umma katika mji mkuu wa Kituruki.

Tunc alisema kwamba watuhumiwa Faruk Koca, S.Y.S. na K.C. walizuiliwa kwa "kumjeruhi afisa wa serikali katika uwanja wa michezo kwa njia iliyosababisha uharibifu" kwani Meler, ambaye pia alihesabiwa kama afisa wa umma, alikuwa akitekeleza majukumu yake uwanjani.

Baada ya bao la kusawazisha katika muda wa majeruhi, Ankaragucu yenye wachezaji 10 walishikwa sare ya 1-1 na wageni Caykur Rizespor katika mechi ya Jumatatu ya Trendyol Super Lig.

Baada ya kipenga cha mwisho, Koca aliingia uwanjani na kumpiga Meler, mwamuzi mwenye leseni ya FIFA, usoni. Mwamuzi alipoanguka chini, watu kadhaa pia walimpiga teke. Baada ya shambulizi hilo, Meler alipelekwa hospitalini Ankara.

Maelezo rasmi

Rais Recep Tayyip Erdogan alikemea shambulizi dhidi ya mwamuzi huyo hapo awali.

"Ninakemea shambulizi dhidi ya mwamuzi Halil Umut Meler baada ya mechi ya MKE Ankaragucu dhidi ya Caykur Rizespor iliyopigwa jioni hii, na ninamtakia uponaji wa haraka,"

Rais Recep Tayyip Erdogan

"Michezo inamaanisha amani na udugu. Michezo haina uwiano na vurugu. Hatutawahi kuruhusu vurugu kutokea katika michezo ya Kituruki," Erdogan aliongeza.

Rais Erdogan alitoa rambirambi zake kwa mwamuzi Meler kupitia simu, akieleza masikitiko yake kwa tukio hilo, na kuagiza mawaziri husika kuchukua hatua muhimu haraka, kama ilivyoelezwa na Idara ya Mawasiliano ya Rais.

Shirikisho la Soka la Uturuki limesimamisha mechi zote za ligi hadi pale watakapotoa taarifa zaidi.

FIFA yakemea shambulizi

Shirikisho la soka duniani FIFA pia lilitoa tamko siku ya Jumanne likikemea shambulizi hilo.

"Hakuna nafasi kwa vurugu katika soka, iwe uwanjani au nje ya uwanja," Rais wa FIFA Gianni Infantino alisema kwenye Instagram.

"Matukio yaliyofuatia mechi ya Ligi Kuu ya Uturuki kati ya MKE Ankaragucu na Caykur Rizespor hayakubaliki kabisa na hayana nafasi katika mchezo wetu au jamii," Infantino alisema.

Meler, mwenye umri wa miaka 37, ni mmoja wa waamuzi wa UEFA Elite na FIFA wanaosimamia mechi kadhaa katika mashindano ya klabu ya UEFA na timu za taifa, ikiwa ni pamoja na Ligi ya Mabingwa wa daraja la juu, pamoja na mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA 2022.

TRT World