Soka la uhispania limekumbwa na mzozo na msukosuko tangu rais wa shirikisho la soka Rubiales alipombusu mdomoni kwa kulazimisha kiungo Jenni Hermoso mbele ya vyombo vya habari duniani kufuatia ushindi wa Uhispania dhidi ya England katika fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake Agosti 20 huko Australia.
"Hawaji tena," shirika la habari la AFP iliambiwa saa chache tu kabla ya kocha mpya Montse Tome kukitaja kikosi chake siku ya Ijumaa kwa minajili ya mechi za Ligi ya Mataifa dhidi ya Sweden na Uswizi mnamo Septemba 22 na 26.
Aidha, mwezi uliopita wachezaji 81 wa Uhispania, wakiwemo 23 wa kikosi cha mabingwa wa dunia, walitoa barua waliosaini huku ikisema hawataichezea timu ya taifa bila mabadiliko makubwa kutekelezwa kwenye uongozi wa shirikisho hilo la soka.
Tangu mgomo huo Rubiales alijiuzulu na shirikisho la soka lilimfukuza kocha wa zamani mwenye utata Jorge Vilda, na badala yake kumuajiri Tome huku ikiahidi mageuzi zaidi ya ndani. Tome alikuwa naibu Meneja wa zamani wa Vilda.
Vyombo vya habari vya Uhispania vilisema kuwa wachezaji hao wanatarajiwa kutoa taarifa baadaye ijumaa ili kuelezea mabadiliko wanayotarajia kuyaona kabla ya kurudi uwanjani.
Wakati huo huo, Rubiales alitarajiwa kufika mbele ya jaji wa Mahakama kuu Ijumaa juu ya malalamiko ya unyanyasaji wa kijinsia uliotokana na busu inayodaiwa kuwa ya lazima kwenye midomo ya Hermoso.