Timu ya Taifa ya Soka ya Palestina itachuana na Lebanon siku ya Alhamisi kabla ya kucheza dhidi ya Australia tarehe 21 Novemba licha ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanayoendelea.
Ushindi wa timu hiyo dhidi ya Lebanon katika Milki za Kiarabu utawapa motisha wachezaji hao huku wakielekea katika hatua itakayofuata.
Aidha, mchuano wa Palestina dhidi ya Lebanon pia umehamishwa kutoka Beirut kwa sababu za kiusalama.
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Palestina Makram Dabboub, ambaye anatoka Tunisia, amekiri itakuwa vigumu kwa wachezaji kuzingatia soka huku familia za wachezaji wengi zikiwa hatarini.
"Wachezaji wako katika hali ngumu kisaikolojia kufuatia vifo na uharibifu huko Gaza. Wengi wa wapendwa wao wa karibu wamekufa kutokana na mabomu," Dabboub alisema.
Awali, Palestina ilikuwa imeratibiwa kuwa mwenyeji wa Australia mechi ya raundi hii ya kufuzu, lakini mchezo huo umehamishwa nchini Kuwait.
Mwezi uliopita, maandalizi ya timu hiyo yalikatizwa kwani wachezaji hawakuweza kuondoka kushiriki mashindano nchini Malaysia.
Kwa sasa timu hiyo iko nchini Jordan ili kuwa na uhakika wa kuwa na uwezo wa kusafiri kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Shirikisho la Soka la Palestina limekuwa mwanachama kamili wa Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA, mwaka 1998 na kimefanikiwa katika ngazi ya kikanda.
Timu hiyo kwa sasa iko katika nafasi ya 96 katika orodha ya hivi karibuni ya viwango bora ya FIFA kwa timu za taifa. Nafasi yake ya juu iliyowahi kufika kwenye orodha hiyo ya FIFA ni 73, iliyosajili mnamo 2018.