Uwakilishi wa Bara la Afrika kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia umeongezwa kutoka timu tano hadi tisa kwenye Kombe la Dunia la 2026 baada ya FIFA kupanua washiriki hadi timu 48.
Hii imetoa motisha ya ziada wakati wa kufuzu, ambayo itaendelea hadi Oktoba 2025.
Nafasi hizo tisa za kufuzu moja kwa moja zinatarajiwa kuwa na ushindano mkali kati ya timu za bara la Afrika.
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” tayari kimefunga safari ya kuelekea Morocco kuchuana na Niger mechi ya kundi E kufuzu Kombe la Dunia.
Kipute hicho kimeratibiwa kupepetwa katika uwanja wa Marrakech Grand, ulioko mjini Marrakech, siku ya Jumamosi, tarehe 18 Novemba, 2023.
Aidha, Uganda itakutana na Guinea Ijumaa, tarehe 17 Novemba 2023 katika uwanja wa Stade De Municipal mjini Berkene kabla ya kuminyana na Somalia katika uwanja huo huo siku nne baadaye zikiwa ni mechi za Kundi G.
Aidha, timu ya Keya ya Harambee Stars iliondoka siku ya Jumatano kuelekea Gabon tayari kukabiliana na Gabon katika mechi yake ya ufunguzi ya kufuzu, kundi F, Alhamisi, Novemba 16, 2023.
Wakufunzi wa timu zote za Kenya, Uganda na Tanzania wamevitaja vikosi vyao tayari kwa safari hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Jijini Dar es Salaam, Tanzania, timu ya taifa ya Soka ya Burundi itachuana na The Gambia leo alasiri mechi ya kufuzu (Kundi F).