Soka ya Tanzania imeifanya ligi yake na vilabu vyake kuwa mfano bora na kuwa kivutio kwa wachezaji na makocha wa kigeni ikilinganishwa na ligi nyingine Afrika Mashariki, lakini kwa nini? TRT Afrika inakuletea uchambuzi wa kina kuhusu hilo.
Tanzania, imekuwa ni kivutio kikubwa kwa wanasoka na makocha kutoka mabara tofauti, likiwemo bara la Ulaya na Amerika ya Kusini.
Taarifa ya Shirikisho la kimataifa la historia na takwimu za mpira wa miguu (IFFHS), iliitangaza ligi ya Tanzania bara kuwa ya tano kwa ubora barani Afrika mwaka 2022.
Wanasoka wengi wanatamani kucheza mpira wa kulipwa nchini Tanzania kwa sababu ya mishahara minono, uhakika wa malipo, ushabiki mkubwa wa wapenzi wa soka na ukubwa wa vilabu vyenyewe wanavyovichezea barani Afrika.
Licha ya ukweli kwamba Kenya na Uganda zimekuwa katika viwango vya juu kwenye jedwali la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), hata hivyo nchi hizo bado zimeshindwa kuwa na hamasa na uwekezaji kama wa Tanzania.
Ndani ya kipindi cha takriban miaka mitano, uwekezaji mkubwa umeshuhudiwa katika kandanda ya Bongo ( Tanzania), huku mabilioni ya shilingi yakibadilishana mikono katika udhamini, kuanzia ngazi ya vilabu na ligi kwa ujumla.
Vilabu mbalimbali vikiwemo watani wajadi Simba, Yanga na Azam FC, vimewekeza pakubwa katika soka ya nchi hiyo.
Aidha, uwekezaji wa matajiri mbalimbali unaofanywa nchini Tanzania umevipa na kuviongezea thamani vilabu mbalimbali, vikiwemo Singida Fountain Gate, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na timu nyinginezo.
Usajili huo, unaotokana na uwekezaji wa MO uliotajwa kuifanya Simba iliyofika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, kukadiriwa kuwa na thamani kubwa zaidi ya takriban bilioni 5.69, kwa mujbu wa mtandao wa ‘transfermarket’.
Usimamizi wa klabu ya Simba umenukuliwa ukisema kuwa haushindwi kumsajili mchezaji yoyote unaomtaka hasa kutoka katika ukanda huu wa Afrika sababu tu ya jeuri ya pesa ya mwekezaji wake Mohamed Dewji, maarufu kama MO, ambaye mara nyingi amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa vijana barani Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya jarida la Forbes, Dewji, ambaye anakadiriwa kuwa na umri usiozidi miaka 48, ana utajiri wa dola za Kimarekani 1.5 ( wastani wa shilingi za Kitanzani trilioni 3.4) zinazomfanya kuwa tajiri wa 15 Afrika.
Uwekezaji wa Mo Dewji umeifanya Simba kuongoza orodha ya vilabu vinne vyenye thamani kubwa zaidi nchini Tanzania huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Yanga (TZS bilioni 5.49), Azam FC (TZS bilioni 2.68) na Namungo FC (TZS milioni 510.85).
Aidha, Klabu ya Yanga, inayomilikiwa na bilionea Gharib Said Mohamed, maarufu GSM, pia imekuwa ikiwasajili wachezaji maarufu na makocha kutoka nje ya Tanzania, ikiwemo kutoka bara la Ulaya.
Wengine ni mawinga Skudu Makudubela ( Afrika Kusini), Maxi Mpia Nzengeli, Jesus Moloko (Congo DRC), Kennedy Musonda (Zambia) na Hafiz Konkoni kutoka Ghana.
Kulingana na Afisa Habari wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Clifford Ndimbo, mazingira mazuri yaliyowekwa, yamevutia uwekezezaji endelevu kwenye ligi hiyo.
“Ligi yetu imekuwa ligi bora na yeye thamani kubwa ukilinganisha na ligi nyingine ikiwemo ya Kenya na Uganda sababu ya uwekezaji na mazingira bora,”anasema Ndimbo.
Miaka mitatu iliyopita, Azam Media, inayomilikiwa na Said Bakhressa, ilisaini na kuwekeza kiasi cha bilioni 225.6 shilingi za Kitanzania kwa kipindi cha miaka 10 ikiwa na haki miliki za ligi hiyo, ikiwemo kuonyesha mechi katika ving’amuzi vyake vya Azam TV.
Aidha, sapoti kubwa na motisha inayotolewa na Serikali ni moja ya sababu ya ukuaji wa soka ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa hamasa kubwa, ikiwemo ya kuwakabidhi pesa kama motisha kwa Simba, Yanga na timu ya Taifa.
Juhudi za Tanzania za kuwekeza kwenye soka lake, hazijaambulia patupu. Taifa Stars ndio timu pekee iliyofuzu Michuano ya AFCON 2024 kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa ni mara yake ya tatu katika historia.
Baada ya Stars kufuzu, Serikali ya Tanzania ilitoa shilingi milioni 500 kama sehemu ya pongezi na wakati mwingine imekuwa ikitoa hadi ndege kusafirisha timu kwenda nje katika michuano ya kimataifa.
Ingawa Tanzania iko nafasi ya 122, nyuma ya Kenya iliyopo nafasi ya 109, na Uganda 89 katika viwango vilivyotolewa na FIFA mnamo mwezi Septemba, 2023, nchi hizo zimeshindwa kujikatia tiketi ya kufuzu fainali za AFCON zitakazofanyika Ivory Coast mwakani.
Hii itakuwa ni mara ya tatu Tanzania kufuzu AFCON baada ya kuwahi kufanya hivyo mara ya mwisho 2019 chini ya kocha Mnigeria Emmanuel Amunike na mwaka wa 1980 ilipokuwa chini ya kocha Joel Brndera, ambaye baadae aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo ya Uwaziri wa Michezo.
Na Nuri Aden na Selemani Jongo