Wenyeji Kenya na Rwanda walijinyakulia nafasi za kushiriki nusu fainali baada ya kutwaa nafasi mbili bora za kwanza katika kundi A.
Kenya ilimaliza kileleni mwa Kundi A na kudumisha fomu ya kushinda mechi zake zote 100% baada ya kuikung'uta Somalia 4-1.
Rwanda, Amavumbi ilifuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga Sudan mabao 3-0 Katika mechi ya Kundi A iliyochezwa ugani Jomo Kenyatta siku ya Ijumaa.
Mechi za nusu fainali zimeratibiwa kugaragazwa Uwanja wa Jomo Kenyatta, mjini Kisumu nchini Kenya tarehe 5 Disemba.
Baada ya Tanzania na Zanzibar kuwa sawa kwenye idadi ya alama (4) kila mmoja na pia kufunga idadi sawa ya mabao, vigezo vya nidhamu vilitumika huku Tanzania ikifuzu kwa kuwa na maonyo manne dhidi ya Zanzibar iliyoshuhudia maonyo matano.
Wenyeji Kenya wanatarajiwa kuwategemea motisha ya mashabiki wa nyumbani watakapochuana na Tanzania huku Uganda ikikabiliana na Rwanda kwenye mechi hizo za kufana za nusu fainali.
Michuano hiyo ya Cecafa U-18 kwa wavulana, ambayo imevutia jumla ya timu nane, itafikia kilele tarehe 8 Desemba, 2023.