Katika kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg, Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, na Wadau mbalimbali inaendelea kutekeleza mikakati ya uelimishaji na uhamasishaji jamii.
Serikali hiyo imewatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa kuwajengea uwezo wahudumu wapatao 1322 ambapo kati yao Wahudumu wanatoka Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mjini na vijijini.
Sambamba na hilo serikali ya Tanzania, pia imetoa magari 8 maalum ya matangazo kwa ajili ya utoaji wa elimu ya Ugonjwa wa Marburg katika maeneo mbalimbali hususan sehemu zenye mikusanyiko.
Katika kuhakikisha kila mtu anaufahamu Tanzania imewajengea uwezo viongozi mbalimbali wa dini ili waweze kuelimisha jamii katika nyumba zao za ibada ambapo takribani viongozi wa dini 310 wamepewa elimu ya uhamasishaji mkoani Kagera eneo ambalo liliathirika na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa wizara ya Afya Tanzania tayari shule zote zimeweza kupatiwa elimu pamoja Taasisi zingine ikiwemo magereza, sehemu za Ulinzi na Usalama ikiwemo jeshini na vielelezo vyote vya kutolea elimu vimekuwa vikitolewa kwenye taasisi hizo kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross Society)
Ugonjwa wa homa ya Marburg ulioripotiwa rasmi nchini Tanzania mnamo tarehe 21 Machi, 2023 mkoani Kagera. Mpaka kufikia sasa serikali ya Tanzania imetoa taarifa rsmi kuwa hakuna wagonjwa wapya.