Meli ya MV Logos. Picha: Mamlaka ya Bandari ya Kenya

Maktaba kubwa zaidi ya kuelea duniani yenye vitabu zaidi ya mada 5,000, imetia nanga katika Bandari ya Mombasa Kenya ambapo ilikaribishwa na mamlaka ya bandari ya Kenya iliposafiri kupitia mlango wa bahari wa kilindini na kutia nanga kwenye geti ya Mbaraki ndani ya bandari hiyo.

Kwa wastani, wageni milioni moja wamepokewa kwenye meli hiyo ya matakaba ya kuelea kila mwaka huku maonyesho ya vitabu yanayoelea yakiwapa wageni wengi fursa ya kununua vitabu.

Meli hiyo ya MV logos ina uwezo wa kubeba tani 12,519 na abiria 350 pamoja na kuwa na urefu wa jumla wa mita 132.5 na upana wa 20.8, na kimo cha mita 5.2 ndani ya maji.

MV logos itafunguliwa kwa Umma kwa muda wa siku 45 huku wakitarajiwa kufurahishwa kwa kuzuru ndani ya meli hiyo kubwa ili kugundua huduma mbalimbali za kufana zinazopatikana ndani yake kama vile mkahawa wa kimataifa, sitaha ya wageni, eneo la mapokezi miongoni mwa zingine.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya Kapteni William Ruto amesifu ziara ya MV Logos Hope katika bandari ya Mombasa huku akisema kuwa ziara hiyo ya aina yake inaashiria kuwa Kenya imepiga hatua kubwa katika kurejesha nafasi yake kama kitovu cha meli katika saketi ya bahari ya Hindi.

Meli ya MV Logos Hope itaondoka Mombasa na kuwasili Dar Es Salaam, Tanzania tarehe 5 Oktoba 2023 ambapo itakaa hadi tarehe 23 Okt 2023.

TRT Afrika