Wakazi wa mji wa Mombasa, nchini Kenya wamejitokeza mwishoni mwa juma katika eneo la Jomvi Miritini na kupanda miche zaidi ya 4000 ya mikoko. 

Wenyeji wa mji wa Mombasa, nchini Kenya wamepanda zaidi ya miche 4000 ya mikoko. Wakazi hao walijitokeza mwishoni mwa juma katika eneo la Jomvu Miritini wakishirikiana na wadau wengine kutoka nje ya nchi ikiwemo Brazil katika upandaji miti huo.

“Tumepanda zaidi ya miche elfu 30 katika kipindi cha miaka 3. Tunashukuru kwamba kuna sehemu ambayo tayari imeota na ndio maana leo tumesogea sehemu nyengine na kupanda miche 4400.”

Joy Koech kutoka Blue Earth

Hatua hii ambayo imeanzishwa na wadau mbalimbali wa mazingira ni katika jitihada zinazofanywa na wakazi wa eneo hilo la Pwani kukabiliana na tishio la kutoweka kwa mikoko katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki.

Mikoko ambayo ni miti ya asili inayoota pembezoni mwa fukwe za bahari, tafiti zimethibitisha kuwa na umuhimu mkubwa katika kuzuia kasi ya mawimbi ya bahari yanayosababisha mmomonyoko wa ardhi pembezoni. Mbali na hivyo, mikoko pia hutoa mazingira rafiki kwa samaki kuzaliana.

Mikoko ni miongoni mwa miti inayotoweka kwa kasi dunia hivyo kusababisha athari kubwa katika ikolojia pamoja na jamii.

Tafiti za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa, mikoko ndio miti inayotoweka kwa kasi zaidi duniani kuliko miti mengine. HiIo limesababisha athari kubwa kwa ikolojia na uchumi kwa ujumla.

Joy Koech ambaye ni mwanzilishi wa shirika la mazingira la Blue Earth pamoja na wadau wengine wa mazingira walioratibu shughuli hiyo ya upandaji mikoko anasema juhudi hizo ni za kuitumikia jamii.

“Tumepanda zaidi ya miche elfu 30 katika kipindi cha miaka 3. Tunashukuru kwamba kuna sehemu ambayo tayari imeota na ndio maana leo tumesogea sehemu nyengine na kupanda miche 4400,” anasema Joy.

Mikoko imesifiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi hewa ya ukaa yani carbondioxide kutoka angani na kuzalisha oksijeni ambayo hutumiwa na viumbe hai.

Sifa nyengine ya mikoko ni uwezo wake wa kuchuja na kuondoa asilimia 90 ya chumvi iiyopo katika maji ya bahari kuingia kwenye mizizi yake.

Nae Athumani Mwamiri ambae pia ni mmoja wa waratibu wa zoezi hili, anasema licha ya sifa hizo za mikoko, lakini ubora wake wa kukaa miaka mingi bila kuoza ndio umekuwa ponza, kwani hutumiwa zaidi kwa shughuli za ujenzi, hivyo kuiweka hatarini kutoweka.

Muendelezo wa jitihada hizi, huenda zikazaa matunda hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo mvua nyingi ambazo zinaweza kuleta mafuriko na athari nyengine.

TRT Afrika