Allen The Dapper: Nyota wa filamu na mitindo ing'aayo nchini Kenya

Allen The Dapper: Nyota wa filamu na mitindo ing'aayo nchini Kenya

Mwanamitindo huyu amejizoelea umaarufu mkubwa katika kuwaremba wateja wake.
Allen anajulikana kama Dapper, amekuwa mashuhuri kupitina mitindo na filamu. Picha: Grafiki

Mitindo ya kijasiri na ya kipekee. Hivi ndivyo mwanamitindo maarufu wa Kenya Allen ‘the Dapper’ Igatanyi anavyofafanua mtindo wake.

Ubunifu wake wa kipekee umemletea umaarufu katika ulingo wa mitindo Kenya, huku baadhi ya watu maarufu katika tasnia ya muziki - Mejja, Otile Brown na wasanii wa gengetone Ethic - wakiwa wamevalia chapa yake ya mavazi ya kipekee, ‘’FALA Wear’’.

Lakini si watu wengi wanaojua kuwa chapa hiyo iliyopata umaarufu - ilianza na Allen kubadilisha moja ya mavazi ya ofisi ya marehemu mama yake kuwa ya rangi ya kuvutia yenye msokoto wa Kiafrika.

"Ilikuwa suti ya suruali ya bluu ambayo niliikata haraka ili kutengeneza kaptula," anaiambia TRT Afrika. "Pia nilikata mikono ya koti kisha kuweka kitambaa cha maandishi ya Kiafrika nyuma na pia kwenye mikunjo ya koti - kifuani."

Fesheni ya Kifala

Huu ulikuwa ni moja kati ya miundo iliyompa jina ‘fala’ - maana yake ‘mpumbavu’ katika lugha ya mtaani Kenya.

"Siku zote nilikuwa mvulana huyo aliyevaa nguo za kiafrika za kuvutia. Watu wakiniona nikija na kusema, cheki yule fala (mtazame mpumbavu huyo),” Allen, 29, anakumbuka huku akitabasamu. "Kwa hivyo nilifikiria, kwa nini nisibadilishe jina hilo kuwa kitu chanya na kulitumia kama chapa yangu? Na hivyo ndivyo Fala Wear alizaliwa mnamo 2015.

Jina la - 'dapper' pia ina asili ya kuvutia.

“Hilo jina kweli lilitoka kwa mchungaji kanisani. Alipokuwa akihubiri kwenye mkutano, alininyooshea kidole na kusema, 'Mungu anapenda watu ambao ni safi na wanaofanana na mvulana huyu.' Nikaipenda hio jina na hadi leo limenisakama.”

Allen baadaye angejiandikisha katika Taasisi ya Buruburu ya Sanaa Nzuri (BIFA) katika mji mkuu, Nairobi, lakini aliacha shule haraka ili kuzingatia kikamilifu miundo yake mwenyewe.

"Uzoefu wangu katika BIFA ulikuwa mzuri lakini sikudumu hata wiki, kwa sababu haikuwa na maana kwangu kukaa darasani, kusikiliza somo kuhusu mitindo wakati ningeweza kujifunza zaidi kwa kufanya kazi katika tasnia hiyo."

Allen the Dapper, ameijipatia umaarufu kupitia nguo za mama yake. /Picha: Allen

Kamera-tayari

Tamasha lake la kwanza la urembo liliishia kuwa maonyesho iliyorikodiwa na video za muziki - kulingana na Allen, tajriba hio ilimlipa zaidi kuliko hata pesa aliyotarajia kulipwa.

"Katika maoneysho hayo, ilibidi nivalishe watu wote, na hiyo ilikuwa ngumu kwa sababu sikuwa na timu ya wanamitindo ambayo inaweza kunisaidia kuweka mavazi ya sare. Kufanya yote hayo na kutolipwa mwishowe kulinivunja moyo.”

Fursa hiyo hata hivyo, ilimfungulia njia ya kuanzisha mitindo yenye maridadi zaidi ambayo hatua kwa hatua ilimsaidia kuanzisha chapa yake. Mapumziko yake makubwa yalikuja wakati fursa ya kumtengeneza Jimmy Gait - mmoja wa wasanii wakubwa wa injili wa Kenya wakati huo - ilipofunguliwa.

"Video hiyo ilikuwa maarufu na ilikuwa muhimu kwangu kama mtunzi, kwa sababu kwa namna fulani niliweza kuwa sehemu ya wimbo huu maarufu," Allen anasema.

"Ghafla wasanii wengine wengi na hata watu wengine kwa ujumla walitaka kufanya kazi na mimi na kununua miundo yangu. Hii ilinifungulia fursa zaidi ya kushirikiana na mashirika mengine ya mitindo.

Hali ya mtu Mashuhuri

Kuwatayarisha wasanii ili warikodiwe na kamera, na kufanya kazi kwa ukaribu na wataalamu wa filamu na TV, pia kulimpa Allen fursa ya kukuza kipawa chake kingine - uigizaji.

Uigizaji ulienda vyema na ustadi wake wa mitindo, ilimpandisha juu hadhi yake kama mtu mashuhuri na hatimaye ikampa nafasi kwenye kipindi maarufu cha uhalisia kinachoenyeshwa na Showmax Afrika Kusini Showmax.

Tajriba hii ilimfundisha somo muhimu katika kuifahamu zaidi usanii wake wa kubuni, huku akifanya kazi na wateja mbalimbali.

"Ni muhimu kila wakati kusikiliza silika yako na kuwa mjasiri kupambana na yatakayotekea," anasema. “Kufanya kazi za uanamitindo kumenipelekea kupata fursa nyingi sana ambazo nazishukuru. Nimejifunza kwamba kwa kadiri mteja anavyokuwa sahihi kila wakati, ni muhimu pia kujiamini na kutoruhusu mtu yeyote kuchukua fursa ya sanaa yako.”

Allen anaamini kuwa mtazamo huu umemsaidia kumpa motisha haswa katika taaluma ya mitindo.

"Nataka kuunda mtindo ambao unaweza kumfurahisha mtu wakati ana huzuni; mtindo unaompa mtu ujasiri wa kuendelea,” asema. "Matumaini yangu siku moja ni kuwa mavazi yangu yatapatikana na kila mtu."

TRT Afrika
Tovuti hii hutumia vidakuzi. Kwa kuendelea kuangalia tovuti hii, unakubaliana na utumizi wa vidakuziSera ya Vidakuzi
Kubali