Baada ya Joola kupinduka iliendelea kuonekana juu ya maji kwa saa 16 kabla ya kuzama. Picha: Nyingine

Na Charles MgboluIlikuwa saa 11 usiku mnamo Septemba 26, 2002, feri pekee nyeupe ikiwa na abiria 1,800 hivi karibu na pwani ya Gambia ilivuka kwenye dhoruba hatari kwenye Bahari ya Atlantiki.

Upepo na mvua vilikumba chombo hicho, na mawimbi makali yalilivamia upande wake, likilipigapiga kama mchezo wa kifo na kuwaacha abiria waliogopa wakipiga yowe kwa hofu.

Feri hiyo ilikuwa Joola, meli ya baharini iliyo milikiwa na Senegal iliyotoka bandarini mwa Ziguinchor katika eneo la Casamance kusini mwa Senegal saa 7:30 mchana siku hiyo ya kusikitisha kwa safari ya masaa 17. Mwisho wa safari ilikuwa mji mkuu, Dakar, na kusimama kwa muda mfupi kisiwani Carabane

Joola ilisafiri mbali zaidi baharini kuliko ilivyokuwa na leseni ya kufanya na haikuwa na nafasi dhidi ya dhoruba kubwa kama hiyo.

Dakika tano baada ya kuingia na kukumbwa na dhoruba, feri hiyo ilipata shida, ikageuka upande na kuzama kwenye mawimbi makubwa.

Rekodi rasmi zinaeleza watu 1,863 walizama kwenye janga hilo, na walionusurika ni 64 pekee.

Bado ni janga kubwa zaidi la baharini nchini Senegal na inatambuliwa kama janga la tatu kubwa zaidi la baharini katika historia ya majini, ikizidi idadi ya vifo vya Titanic ya zaidi ya 1,500 mwaka 1912.

Wakhani alipoteza familia na marafiki katika ajali hiyo. Picha: Wakhani Sambou

"Nilitakiwa kuwa kwenye chombo hicho. Nilipaswa kuwa nao, lakini nilikuwa nacheza mpira wa miguu Dakar," Wakhani Johnson Sambou, mwandishi wa habari Msenegali ambaye alipoteza ndugu na marafiki wengi, anaiambia TRT Afrika kabla ya maadhimisho ya mwaka wa 21 ya janga hilo.

Miongoni mwa wanafunzi wengi waliozamishwa na vilindi vya bahari usiku huo, wengi wao walikuwa wanachama wa timu ya vijana ya mpira wa miguu iliyokuwa ikielekea mji mkuu wa kitaifa kushiriki mashindano.

"Kuna wanafunzi wengi walikufa kwa sababu ilikuwa mwanzo wa mwaka wa masomo; baadhi yao walikuwa wakielekea mji mkuu, Dakar, kwa kuanza kipindi kipya cha masomo," anasimulia Wakhani.

"Niliwapoteza marafiki zangu wawili bora. Walikuwa kwenye chombo kwa mara ya kwanza na dada yao mdogo. Miili yao haikupatikana kamwe."

Uzembe

Uchunguzi ulioanzishwa na serikali ya Senegal ulitaja kwa kiasi kikubwa janga hilo kuwa ni makosa ya kibinadamu na uzembe, lakini hakuna aliyepelekwa mahakamani hadi sasa.

Idadi ya abiria ilikuwa zaidi ya mara nne ya uwezo wa kubeba wa feri hiyo, wengi wao wakiwa sehemu mbalimbali za meli hiyo.

Na idadi kubwa kama hiyo ya abiria, ilikuwa haiwezekani kwa nahodha, ambaye pia alipoteza maisha katika janga hilo, kudhibiti chombo kisizame wakati kilipambana na dhoruba.

Mashuhuda wanasema baada ya feri kugeuka, watu waliokwama kwenye matundu ya hewa chini ya chombo walizidi kupiga yowe kwa msaada hadi hatimaye kuzama mita 20 kwenye maji kama masaa 16 baadaye.

Kumbukumbu kwa waathirika

"Juhudi za uokoaji wakati huo hazikuwa za kutosha. Wakati waokoaji walipofika kwenye feri hiyo, hawakuwa na vifaa vya kisasa vya kuokoa watu wengi kwa muda mfupi sana," anasema Ibrahima Gassama, mwandishi wa habari Msenegali mwingine ambaye ameandika sana kuhusu janga la Joola.

Makumbusho kwa heshima ya waathirika wa janga hilo inajengwa huko Ziguinchor, ikizungukwa na barabara yenye shughuli nyingi na Mto wa Casamance. Makandarasi wanakimbia ili kukamilisha mradi huo ifikapo mwisho wa mwaka.

Lakini Gassama anasema familia za waathirika wanataka zaidi ya makumbusho tu.

"Wanataka mabaki ya feri yavutwe kutoka baharini. Hii ndiyo njia pekee kwa wengi kupata faraja na kupona. Wanataka feri iwe kwenye makumbusho, ili wapendwa wao waliotangulia mbele ya haki wapewe hati ya mwisho."

Serikali imesema bado haijafaulu kufanikisha hili kutokana na changamoto za kiufundi.

"Kuna wasiwasi pia kutoka kwa baadhi ya Wasenegali kwamba kutoa chombo kutakuwa janga lingine kwa sababu litaibua mengi hususani kuibua maumivu mapya kwa waathirika.

Hivyo, je, Senegal imejifunza kutokana na janga hili la kutisha? Gassama hafikiri hivyo.

"Siku baada ya kuzama kwa meli, sisi kama Wasenegali tulisema, kamwe tena, na tabia zilibadilika, lakini ilidumu tu kwa wiki. Wasenegali wamerudi kwenye mazoea yao ya zamani," anasema kwa TRT Afrika.

Majanga yanayosubiri kutokea

Hili ni kweli hasa kwa sababu ya kuvuka kwa wahamiaji haramu baharini kuelekea Atlantiki lililoshika taifa la Afrika Magharibi kama homa.

Kama ilivyokuwa kwa Joola, vijana wengi wa Senegal bado wanakufa baharini baada ya kujazana kwenye boti duni zenye mizigo mizito ambazo mara nyingi huzama kati ya njia kuelekea mataifa ya Magharibi baada ya kusafiri kwenye dhoruba.

Mamia ya wahamiaji wa Senegal wamekufa maji walipokuwa wakisafiri kwa boti zilizojaa watu. Picha: Reuters

Ajali ya boti ya hivi karibuni zaidi ilitokea Agosti mwaka huu ambapo zaidi ya Wasenegali 60 walizama au pwani ya Cape Verde walipokuwa wakijaribu kufikia Ulaya, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

Katika siku na miezi iliyofuata janga la Joola, kulikuwa na kampeni nyingi za kuwaelimisha watu kuhusu hatari ya msongamano wa abiria kwenye vyombo vya majini.

Gassama anasema ni kushangaza kwamba watu wanashindwa kutumia hili katika maisha yao ya kila siku.

"Nchini Senegal, mabasi ya usafiri yanajazwa kupita kiasi, na bado kuna ajali nyingi za magari barabarani, na vifo vingi vinatokana na kuvunja sheria nyingi za usafiri. Kama Wasenegali, tunawezaje kusahau?" anasema.

Mwandishi mwenzake Wakhani anasema. "Watu wasicheze na maisha. Kusafiri kwa bahari, barabarani, au angani vyote ni hatari, na tunapaswa kuheshimu sheria."

Wakhani anafurahi kwamba walionusurika na familia za waathirika wamefanikiwa kuendelea mbele licha ya maumivu ambayo hayapungui.

"Maumivu ya vifo Vya ndugu zao kamwe hayatasahaulika kwa sababu hawakustahili kufa. Lakini nina hakika wote wako kwa amani," anasema.

Wakati kumbukumbu nyingine ya usiku huo wa kuhuzunisha inapoadhimishwa, wale wanaolazimika kuishi na kumbukumbu za jinsi Joola ilivyozama wangeweza kupata faraja kubwa ikiwa wangejua janga lingine kama hilo lisingetokea tena.

TRT Afrika