Saida Karoli./Picha: Wengine

Na Paula Odek

Saida Karoli sio jina geni masikioni ya wapenzi wa muziki katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Nyimbo mbalimbali zilizotungwa na mwanadada huyo kutoka Tanzania, kama vile Maria Salome, Kaisiki, Ndombolo na Mimi Nakupenda, hakika zilikonga nyoyo za mashabiki mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Saida Karoli alizaliwa mnamo tarehe 4 Aprili, mwaka 1976 mkoani Kagera.

Kwa bahati mbaya aliishia elimu ya shule ya msingi, yaani darasa la 5 kutokana na kukosa msaada kutoka kwa baba yake.

Akiwa amekulia kijijini, mila za ukoo wake hazikumruhusu Saida kujihusisha na masuala yoyote ya muziki.

Hata hivyo, mama yake alikuwa na kipaji cha muziki na ndiye alimpa moyo na kumfundisha masuala mbalimbali ya sanaa hiyo, hasa upigaji wa ngoma.

Uwezo wake mkubwa kwenye muziki uligunduliwa na FM Productions waliokuwa mkoani Kagera kusaka vipaji, na moja kwa moja kumpeleka Dar es Salaam ambapo ilimchukua wiki tatu tu, kuachia vibao vikali vilivyotamba ndani na nje ya Tanzania enzi hizo kupitia albamu yake ya Maria Salome aliyoitoa mwaka 2001, akiwa chini ya mzalishaji maarufu wa kipindi hicho aitwaye Mika Mwamba.

Albamu hiyo ilisheheni nyimbo kama vile Maria Salome au Chambua Kama Karanga, ambao ulikuwa na mahadhi ya kihaya.

Ni kupitia kwa albamu ya Maria Salome, Saida aliweza kuzuru nchi mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na kujizolea maelfu ya mashabiki.

Pia alipata fursa ya kutumbuiza mbele ya Mfalme Kabaka wa Buganda.

Mwaka uliofuata, Saida akaachia albamu nyingine yenye jina Mapenzi Kizunguzungu na kufanikiwa kuteka nyoyo za mashabiki wake kama ilivyokuwa kwa Maria Salome.

Baada ya kupotea kwa muda mrefu, Saida Karoli akaibuka tena mwaka 2017 na kibao cha Orugambo ambacho hakikuweza kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Maria Salome na nyinginezo.

Wengi mtakumbuka wimbo wa Salome ulitolewa na Diamond na Rayvanny mwaka 2016 ambao ulikuwa na baadhi ya vionjo kutoka kwenye wimbo wa Saida Karoli uitwao Maria Salome.

Katika mahojiano yake na gazeti moja nchini Tanzania, Saida Karoli mwenyewe alinukuliwa akisema kuwa aliwahi kupata kiasi kisichozidi Dola za Kimarekani 380 baada ya wimbo wake kurudiwa.

Kwa sasa, Saida Karoli amehamishia maskani yake mkoani Mwanza nchini Tanzania ambako ndiko anapofanyia shughuli zake za muziki.

TRT Afrika