Mbwa wa polisi amshambulia mwaandamanaji huko Rotherham, Uingereza, Agosti 4, 2024. REUTERS

Na Abdulwasiu Hassan

Hofu ya kinachoweza kuwatokea kinaweza kuwa kubwa kutokana na uzoefu wa tukio lenyewe linaloogopesha.

Zahara Dattani, Mtanzania anayesimamia nyumba ya wazee huko Uingereza, anapitia hisia hizi za hofu mara tu pale taarifa zinapofika kuhusu wahamiaji walengwa kwenye ghasia zinazoendelea nchini humo.

Anaogopa sio tu kwa usalama wake bali pia kwa wafanyakazi wengi wahamiaji anaowaajiri.

"Nadhani athari ya jumla tunayohisi ni hisia ya kuona kitakachotokea huko mbele ya safari," Dattani anaiambia TRT Afrika.

"Ingawa mimi na wafanyakazi wangu hatujakumbana na waandamanaji, kuona kinachoendelea kote nchini ni kama kusubiri kitu kibaya kitokee kwa wasiwasi."

Mwandamanaji akiwa na moshi huku maafisa wa polisi wakisimama nje ya hoteli moja, huko Rotherham, Uingereza, Agosti 4, 2024. / Picha: Reuters

Ghasia zinazoendelea zilianza zaidi ya wiki moja iliyopita baada ya makundi ya mrengo wa kulia dhidi ya wahamiaji kuchochewa na kile kilichoonekana kuwa uvumi kuhusu asili ya mhalifu aliyeuwa wasichana watatu wadogo kwa kuwachoma visu huko Southport, kaskazini mwa England mnamo Julai 29.

Tangu wakati huo, ghasia zimeendelea bila kupungua katika miji mbalimbali ya Uingereza, huku wahamiaji wa Kiafrika na Asia wakishambuliwa mara kwa mara licha ya onyo la mamlaka kwamba watekelezaji wa vurugu za kibaguzi watachukuliwa hatua.

Katika maeneo kama Belfast, huko Ireland Kaskazini, waandamanaji wa mrengo wa kulia walikuwa wakipiga kelele za chuki dhidi ya Waislamu na biashara za eneo hilo pia zilishambuliwa.

Ghafla, nchi ambayo idadi kubwa ya Waafrika wanahamia imekuwa hatari kwao kuishi. Sio kwamba kila kitu kilikuwa shwari hadi kuzuka kwa ghasia.

Waafrika na Waasia wamekuwa wakilazimika kukabiliana na tuhuma za kwamba wamekuwa wakiiba ajira.

Maafisa wa polisi wanafanya kazi nje ya hoteli wakati wa maandamano ya kupinga uhamiaji huko Rotherham, Agosti 4, 2024. / Picha: Reuters

Kusubiri tu

Kutokana na hali halisi, ahadi ya serikali ya kuimarisha usalama bado haijawashawishi sehemu kubwa ya Waafrika wanaoishi na kufanya kazi nchini Uingereza kwamba dhoruba itapita hivi karibuni.

Tangu Agosti 5, waandamanaji wamepambana na polisi katika matukio kadhaa huko Belfast, Darlington, na Plymouth.

"Inaonekana kama Uingereza ni mahali salama pamoja na polisi kuwepo kila kona ya nchi, lakini hali ni sio nzuri sana kwa sasa," anasema Dattani.

Amechukua hatua kadhaa za kuzuia na kuwafahamisha wafanyakazi wake kwamba wako hatarini na jinsi ya kukabiliana na kinachoendelea kote kwao.

Waafrika wanaohamia Uingereza hufanya kazi katika sekta tofauti, wengine ni wanafunzi. Picha/Reuters

"Imekuwa kawaida kwao kutotoka peke yao usiku, hasa baada ya kazi, na kubeba vitambulisho vyao kila wakati. Baadhi ya wafanyakazi wetu wanafanya kazi za usiku, na wanahitaji kuwa waangalifu," anasema Dattani.

Dr Ishaka Shittu Almustapha, mhadhiri Mnigeria nchini Uingereza, alisema chaguo pekee kwa wahamiaji ni kujificha na kusubiri dhoruba ipite.

"Tunafanya kila tuwezalo kuwazuia watu wetu wasitembee ovyo. Maimamu wanatoa ujumbe uleule — kwamba watu wanapaswa kuwa waangalifu, ikiwa ni pamoja na kutoenda na watoto na wanawake msikitini kwa sasa," anaiambia TRT Afrika.

Mnigeria mwingine anayeishi London, Dr Shamsuddeen Hassan Muhammad, anajisikia salama katika jiji kubwa la Uingereza lakini hataki kujaribu kuwa jasiri.

"Tunabaki ndani zaidi kwa kuwa hii ni kipindi cha likizo na watoto hawako shuleni. Tunapunguza matembezi yetu hadi shughuli muhimu, tukitoka nje kwa ajili ya sala tu. Hii inasaidia kuhakikisha usalama wa familia yetu katika kipindi hiki kisicho tabirika," anasema.

Ushauri kwa wanao safiri

Nigeria, moja ya mataifa ya Kiafrika yenye idadi kubwa ya wahamiaji kutoka bara hilo nchini Uingereza, ilitoa ushauri wa usafiri kwa raia wake wakati vurugu ziliposambaa maeneo mapya baada ya mlipuko wa kwanza wa ghasia kaskazini mwa Uingereza.

"Vurugu zimefikia hatua hatari sana, kama inavyothibitishwa na mashambulizi yaliyoripotiwa dhidi ya maafisa wa usalama na uharibifu wa miundombinu," inasoma taarifa iliyosainiwa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Nigeria, balozi Eche Abu-Obu.

Wanigeria wameshauriwa kuepuka maandamano ya kisiasa na mikusanyiko na maeneo yenye msongamano.

Ubalozi wa Nigeria nchini Uingereza umetoa taarifa nyingine, ukihakikishia wahamiaji kwamba watajulishwa rasmi kuhusu maendeleo yanayojiri.

Ubalozi wa Kenya pia umetoa taarifa ukihimiza watu wote kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki wanaoishi nchini Uingereza na Ireland Kaskazini kuwa makini na kujisajili na ubalozi kupitia tovuti zake.

Picha ya drone inaonyesha waandamanaji wakiandamana nje ya hoteli huku maafisa wa polisi wakilinda eneo hilo huko Rotherham, Uingereza, Agosti 4, 2024, katika kipande hiki cha video kilichopatikana kutoka kwa video ya mitandao ya kijamii. Up North - Yorkshire Live & Breaking News Telegraph/via REUTERS

Wakati ghasia za mrengo wa kulia zikisambaa kote Uingereza, maelfu ya waandamanaji wa kupinga ubaguzi wa rangi pia wamejitokeza barabarani katika miji kadhaa ya Uingereza kupinga maandamano ya vurugu ya mrengo wa kulia.

Waandamanaji walikusanyika katika eneo la Walthamstow la kaskazini mwa London siku ya Jumatano na mikutano kama hiyo ilifanyika Birmingham, Bristol, na Liverpool wakiahidi kupinga waandamanaji wa mrengo wa kulia.

TRT Afrika