Funza

Huku bara la Afrika, na ulimwengu mzima kwa ujumla zikikabiliana na ongezeko la taka ngumu, Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Wadudu (icipe) kimekuja na njia bora ya kudhibiti changamoto hii.

Katika chapisho lao la kisayansi, watafiti hao wanaelezea uwezo wa funza wadogo wajulikanao kitaalamu kama Alphitobius ambao wana uwezo wa kumeng’enya taka ngumu.

“Ingawa mara nyingi tumekuwa tukiwachanganya na funza wa kawaida, jamii hii ina uwezo wa kuharibu taka ngumu. Hata hivyo, hii ni mara ya kwanza kwa viumbe hawa wanaopatikana barani Afrika, kuwa na uwezo wa kufanya jambo hilo,” anaeleza Dkt Fathiya Khamia, Mwanasayansi Mwandamizi kutoka taasisi ya icipe.

Zaidi ya tani milioni 400 za taka ngumu huzalishwa kila mwaka ulimwenguni, huku asilimia 10 zikirejezwa na nyingine kati ya tani milioni 19 hadi 23 zikiishia kwenye maziwa, mito na bahari.

Zisipodhibitiwa vizuri, taka ngumu huwa na athari kubwa kwenye mazingira, binadamu, wanyama na viumbe hai waishio majini ikiwemo Samaki.

Licha ya kuwa inazalisha asilimia tano tu ya taka ngumu, takwimu zinasema kuwa Afrika ndio bara la pili kuathirika zaidi na taka hizi.

Watafiti wa icipe walijaribu uwezo wa funza hao katika kumeng’enya taka hizo. Moja ya taka hizo ni aina ya Polystyrene ambayo hutumika zaidi kwenye uhifadhi wa vyakula vya kwenye plastiki, vikombe na sahani tofauti.

Licha ya uwepo wa njia mbalimbali zitumikazo kurejeleza taka ngumu, bado njia hizi zinaonekana kuwa sio ngumu tu, bali zina madhara kwa matumizi.

“Utafiti wetu unaonesha kuwa minyoo hawa wana uwezo wa kumeng’enya mpaka asilimia 50 ya taka ngumu. Tumeazimia kufanya tafiti zaidi kuelewa mchakato wa namna viumbe hao wanavyoweza kumeng’enya Polystyrene, na iwapo kuna virutubisho vyovyote wanavyovipata,” anabainisha Evalyne Ndotono, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika taasisi ya icipe.

Zaidi ya hayo, wanasayansi watatafiti uwezo wa viumbe hao kuharibu aina mbalimbali za taka ngumu na kuibadilisha kuwa bidhaa muhimu na salama.

"Utafiti wetu unakuza uvumbuzi wa icipe. Tunaweza kutumia maarifa haya kutatua uchafuzi wa taka ngumu, huku pia tukitumia faida za minyoo ya unga, ambao ni sehemu ya idadi ya wadudu wanaoliwa wenye lishe bora," anasema Dkt Abdou Tenkouano, Mkurugenzi Mkuu wa icipe.

Utafiti wa icipe pia huongeza maarifa juu ya urekebishaji wa viumbe - matumizi ya vijidudu kusafisha mfumo wa ikolojia uliochafuliwa na utumizi wa maji chini ya ardhi.

Kituo hicho pia, huchunguza juhudi shirikishi za utafiti na uvumbuzi na wanasayansi wengine, watunga sera na washirika wa tasnia, ili kutumia uwezo kamili wa funza wadogo na viumbe vingine sawa.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa watafiti kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Wadudu (icipe), kilichopo jijini Nairobi.

TRT Afrika