Dkt Faustine Ndugulile kutoka Tanzania, alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Afya Duniani kwa kanda ya Afrika mwezi Agosti mwaka 2024, akitarajiwa kuanza majukumu yake mapya mwezi Februari mwaka 2025.  

Na Sylvia Chebet

Kukulia kijijini nchini Tanzania, kulimsaidia Dkt Faustine Ndugulile kuzitambua changamoto za huduma za afya katika taifa lake.

Vifo vingi vya akina mama na watoto viliashiria kusindwa kwa mfumo wa kukabiliana na kadhia hiyo.

Hali hii ilimuathiri kwa kiasi fulani kijana huyu.

Alichukua maamuzi ya kusomea udaktari ili ajitolee kuokoa uhai wa wengine.

Miongo kadhaa baadaye, akiwa na shahada mbalimbali ikiwemo ya afya ya umma na sheria, Dkt Ndugulile alichukua hatua ya kugombea nafasi nyeti katika Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa kanda ya Afrika.

"Niligundua kuwa nilibanwa sana hapo awali. Nilikuwa nikitumia muda wangu mwingi kutibu watu badala ya kushughulika na matatizo ya kmfumo," aliliambia jopo la mawaziri wa afya kutoka Afrika wakati wa usaili wake.

"Ili kufikia malengo yangu, niliamua kugombea nafasi za kisiasa na kupitia uzoefu wangu kama mbunge na wazirim nimefanikiwa kufikia malengo hayo na kwa sasa shabaha yangu ni kuleta huo ujuzi ndani ya WHO," alisema.

Mchakato huu ulifanyika Agosti 2024 wakati wa Mkutano wa 74 wa WHO kwa kanda ya Afrika katika mji mkuu wa Congo, Brazzaville.

Ndugulile amefariki dunia miezi mitatu kabla ya kushika hatamu ya nafasi yake, mwezi Februari 2025, akiwa na umri wa miaka 55 tu.

Maono kwenye sekta ya afya

Ama kwa hakika, risala aliyoitoa siku hiyo iliamsha hamu ya kusikilizwa zaidi na jopo hilo, hasa kutokana na maono yake ya muarobaini wa sekta ya afya barani Afrika.

Hakika haukuwa mpambano rahisi kwa Ndugulile, Mtanzania ambaye alikuwa akikabiliana na wagombea wengine watatu wenye uzoefu mkubwa ndani ya kuta za shirika la WHO.

Alikuwa akiwania nafasi hiyo pamoja na Ibrahima Socé Fall kutoka Senegal, Boureima Hama Sambo wa Niger na Richard Mihigo wa Rwanda.

Wakati akimpongeza kwa ushindi wake, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alimsifu Ndugulile kwa kujitoa kwake kupambania suala la afya ya umma.

"Dkt Ndugulile aliaminiwa kuingoza WHO Afrika. Hii ni heshima na jukumu kubwa sana. Mimi, pamoja na wenzangu tutakuunga mkono."

Dkt Ndugulile aliamini kuwa WHO Afrika ilihitaji “kiongozi mwenye mageuzi ambaye atakuwa na maono yenye kuangazia mbali ".

Yeye mwenyewe alijiona kama mtu sahihi, hasa kutokana na usuli wake katika taaluma ya utabibu na mwanasiasa ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa TEHAMA na pia mbunge nchini Tanzania.

Uzoefu wake uliongezeka zaidi Kituo cha Udhibiti Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Kwa Dkt Ndugulile, "afya ni siasa, na kwamba siasa bora hutokana na afya bora ya umma ".

Kwa maoni yake mwenyewe, bara la Afrika lilikosa kiunganishi cha watunga sera na wanasiasa wenye kutoa maamuzi ya bajeti na uwekezaji.

"Maono yangu ni kuona bara la Afrika lenye kustawi,"alisema.

Umuhimu wa WHO

Dkt Ndugulile alionesha wasiwasi wake kuhusu kwanini baadhi ya watu walikuwa wakihoji umuhimu wa WHO kwa bara la Afrika.

"WHO bado ina umuhimu wake, ingawa ni muhimu kwa shirika hilo kushughulikia ajenda ya afya barani Afrika," alisema Ndugulile wakati wa usaili huo.

Kwa sasa, bado bara la Afrika haliko kwenye mstari kufikia malengo endelevu ya maendeleo ifikapo 2030.

"Azma yangu ni kuona kuwa malengo haya," alisema.

Miaka sita tu imesalia kufikia malengo hayo, Ndugulile aliazimia kufanya kazi kwa bidi ili kuongeza ufanisi ndani ya WHO.

Zaidi ya nusu ya kusini mwa jangwa la Sahara bado linakosa huduma za afya kwa tu wote.

Hali hii ilimtatiza Dkt Ndugulile.

Haki ya Msingi

Dkt Ndugulile anataka ufadhili endelevu wa huduma za afya na matumizi bora ya rasilimali katika ofisi za WHO na miongoni mwa nchi wanachama.

Je, ni nani atakuwa tayari kuendeleza maono ya Dkt Ndugulile?

TRT Afrika