Visa vya Malaria viliongezeka kwa milioni 16 kati ya 2019 na 2022 kutokana na janga la Covid. / Picha: AP

Na

Sylvia Chebet

Katika hospitali iliyopo katika mji wa Soa, umbali wa kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé, vigelegele vilisikika wakati Noah Ngah mwenye umri wa miezi sita alipokuwa wa kwanza katika kituo hicho kupokea chanjo mpya ya malaria inayoitwa "RTS,S", moja ya chanjo mbili za kipekee zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kulwa wa Noah alikuwa wa pili kupata sindano ya chanjo hiyo inayotokana na protini iliyoundwa upya, ambayo sasa inasambazwa kwa kiasi kikubwa barani Afrika baada ya uzinduzi wa kitaifa nchini Cameroon, nchi iliyo na ugonjwa wa malaria, tarehe 22 Januari.

"Wazazi wengine wana wasiwasi, lakini najua kwamba chanjo ni nzuri kwa watoto," mama wa mapacha hao, Helene Akono, anaiambia TRT Afrika.

Programu ya chanjo ya malaria ya Cameroon inasifiwa kama "hatua ya kihistoria kuelekea chanjo pana dhidi ya moja ya magonjwa hatari zaidi kwa watoto wa Kiafrika".

Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni kundi lililo hatarini zaidi kuathiriwa na malaria. Mwaka 2022, walihesabika kwa karibu asilimia 80 ya vifo vyote vya malaria barani Afrika. Karibu vifo 580,000 vilirekodiwa kote bara hilo katika kipindi hicho.

Naibu mkurugenzi wa CDC Afrika, Dkt. Ahmed Ogwell, anaamini kwamba mara tu dozi za kutosha za chanjo zitakapopatikana, chanjo itakuwa bora zaidi barani humo dhidi ya janga la vimelea vya malaria Plasmodium falciparum.

"Afrika inahitaji kila zana inayoweza kuchangia kupunguza maambukizi na watu kupata maradhi makubwa, pamoja na kupunguza vifo," anaiambia TRT Afrika.

Kuvurugika kutokana na UVIKO

Juhudi za kupambana na malaria zilikuwa zikizaa matunda, na visa vya ugonjwa huo duniani kote vilipungua kwa asilimia 29 kati ya mwaka 2000 na 2019, kabla ya Uviko-19 kutokea na kuvuruga huduma za afya duniani kote.

"Vifo vya malaria vilikuwa vimepungua katika kipindi hicho kwa zaidi ya asilimia 50%, kutokana na upatikanaji mkubwa wa zana za kuzuia na mbinu bora za uchunguzi na matibabu," anasema Prof. Alassane Dicko wa Idara ya Utafiti na Mafunzo ya Malaria katika Chuo Kikuu cha Bamako, Mali.

Janga hilo halikusimamisha tu kupungua kwa kasi kwa visa vya malaria lakini pia kugeuza mafanikio yaliyopatikana kwani mkazo ulihamia kwenye kupambana na ongezeko lisiloisha la virusi vipya vya Uviko.

Visa vya malaria viliongezeka kwa milioni 16 kati ya mwaka 2019 na 2022 - kutoka milioni 233 hadi milioni 249, ongezeko la asilimia 7%.

chanjo ya RTS,S, R21 ya Chuo Kikuu cha Oxford inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. Picha: AFP

Jumuiya ya matibabu ina matumaini kwamba kampeni inayoendelea ya chanjo itapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa malaria.

Awamu ya majaribio nchini Kenya, Ghana na Malawi, ambapo watoto milioni mbili walichanjwa, ilisababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ugonjwa mkali wa malaria na kulazwa hospitalini.

Mshauri maalum wa Baraza la Kupambana na Malaria la Kenya anaona utoaji wa chanjo kama afueni, ingawa siyo "suluhisho la moja kwa moja".

"Inaokoa maisha, ingawa ufanisi wa chanjo siyo 100%. Lakini hata kwa 40%, inaokoa maisha, hasa katika kikundi cha umri ambacho kina uwezekano mkubwa wa kupata malaria kali," anasema.

Kusambaa kwa malaria kwa wingi

Nchini Cameroon, 30% ya mashauriano yote ya kitabibu yanahusiana na malaria, ikionyesha jinsi ugonjwa huo ulivyoenea katika taifa la Afrika ya Kati.

"Kuwa na zana ya kuzuia kama chanjo kutafungulia mfumo wa afya na kusababisha kulazwa hospitalini na vifo vichache," anasema Aurelia Nguyen, afisa mkuu wa programu wa GAVI, muungano wa chanjo duniani.

Nchini Afrika, nchi nyingine 19, ikiwa ni pamoja na Burkina Faso, Liberia, Niger na Sierra Leone, ziko tayari kufuata mfano wa Cameroon na kuanza programu za chanjo za kitaifa.

Mbali na chanjo ya RTS,S iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Uingereza GSK, chanjo ya R21 kutoka Chuo Kikuu cha Oxford inatarajiwa kuingia sokoni hivi karibuni.

Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema kuwa kuwa na chanjo mbili za malaria kutafunga pengo kubwa kati ya mahitaji na usambazaji, kuokoa maisha ya makumi ya maelfu ya watu.

Mabadiliko Yanayosubiriwa ya Utafiti

Dr. Ogwell anabainisha kuwa kuna maslahi yanayokua katika kutengeneza chanjo dhidi ya vimelea, wakati utafiti na maendeleo (R&D) ya awali yangekuwa yamelenga kupambana na virusi.

"Ukweli kwamba tunaenda kutengeneza chanjo kwa vimelea ni hatua kubwa, hasa kwa malaria, kwani inapunguza kulazwa hospitalini na ugonjwa mkali," anasema.

Malaria inayoambukizwa na Mbu aina ya Anopheles inaua hadi watu 600,000 kila mwaka. Picha AP

Akielezea utoaji wa chanjo kama mabadiliko makubwa, anatarajia kwamba kuanza kwa chanjo kabla tu ya msimu wa maambukizi makubwa itapunguza sana gharama za afya .

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kwamba zana za kuzuia za kawaida kama vile vyandarua visiachwe tu kwa sababu chanjo zinapatikana.

Prof Dicko anasema kuna vikwazo vya kushinda kabla Afrika haijafanikiwa kumaliza malaria. "Chanjo za sasa na zana nyingine hazitoshi kufuta malaria haraka," anaiambia TRT Afrika.

"Serikali za Afrika zinahitaji kuongeza uwekezaji katika utafiti wa malaria ili kupata zana zenye ufanisi zaidi za kudhibiti na kumaliza ugonjwa huo."

Katika ngazi ya dunia, watafiti wanafanya kazi kutengeneza chanjo zenye ufanisi zaidi pamoja na dawa bora za kuzuia na matibabu.

Eneo lingine muhimu, kama anavyobainisha Prof Dicko, ni "kubadilisha kijenetiki" mbu ili wasiweze kuambukiza malaria.

TRT Afrika