Viongozi wa kidini, wakiwemo maimamu na makasisi na makundi ya mashirika ya kiraia yamefanya maandamano ya kupinga LGBTQ katika mji wa pwani wa Mombasa nchini Kenya.
“Tunatoa wito kwa rais wetu William Ruto na viongozi wote, kutounga mkono suala hili. Jambo hili ni la kuharibu maadili ya taifa la Kenya, na kusambaratisha heshima ya raia wa Kenya. Tunamuomba alipinge jambo hili na pia tunaliomba bunge lisiliruhusu jambo hili ndani ya nchi yetu ya Kenya,” Katibu Mkuu wa Baraza la maimamu na Wahubiri wa Kenya, maarufu CIPK, Sheikh Muhammad Khalifa, alisema.
Askofu Mkuu Martin Kivuva Musonde wa kanisa la Mombasa alisema kuwa uamuzi wa mahakama kuu ni sawa na kukuza ajenda ya LGBTQ+ Nchini Kenya. "Ni bahati mbaya sana. Ikiwa unahalalisha kitu, inamaanisha unaikuza, " Kivuva alisema.
Maandamano hayo yamejiri baada ya majaji wa Mahakama kuu kuthibitisha kuwa kundi la watu wa mapenzi ya jinsia moja linaruhusiwa kujiandikisha na hata kubatilisha uamuzi wa awali uliokataa usajili wa mashirika ya watu wa jinsia moja nchini Kenya.
"Kuwasajili (vyama vya LGBTQ) inamaanisha unatoa unafufua tabia hiyo. Ukijiunga na klabu ya mpira wa miguu inamaanisha uko tayari kucheza mpira wa miguu, " Kivuva alisema.
Miaka kumi iliyopita, Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yenye jukumu la kusajili mashirika yasiyo ya Kiserikali, ilikataa ombi la kikundi hicho kwa msingi kwamba "inakuza tabia ya jinsia moja.
Mbunge wa Mrengo unaoongoza wa Kenya Kwanza aliyechaguliwa kutoka Mombasa, Mohamed Jicho pevu, aliongoza maandamo hayo.
Mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma, amefadhili sheria, inayoitwa 'Muswada wa Ulinzi wa Familia 2023', ambayo inapendekeza marufuku ya ushoga, uhusiano wa jinsia moja na shughuli na kampeni zozote za LGBTQ.