Mpango wa kuhamisha Israeli kuja Afrika uliitwa "Mpango wa Uganda."
Hili lilikuwa Pendekezo la Katibu wa Kikoloni wa Uingereza Joseph Chamberlain mwaka wa 1903.
Wazo lake wakati huo lilikuwa ni kuunda nchi ya Kiyahudi katika sehemu ya Afrika Mashariki ambayo ilikuwa ni koloni ya Uingereza.
Miaka ya 1888 wakati wa ukoloni, Afrika Mashariki ilikuwa inaitwa Afrika Mashariki ya Uingereza.
"Moja ya rasimu za kwanza za dhana ya Uzayuni ilikuwa kuchagua makao ya kitaifa kwa watu wa Kiyahudi katika ardhi yenu," rais wa Israeli Isaac Herzog alisema katika hafla ya kumkaribisha nchini Kenya alipokuwa katika ziara rasmi Mei mwaka huu," bila shaka uliitwa mpango wa Uganda lakini ulikuwa mpango wa Kenya."
Wazo hilo liliwasilishwa katika kongamano la sita la dunia la Wazayuni huko Basel mwaka 1903 na Theodor Herzl, ambaye alikuwa mwanzilishi wa vuguvugu la kisasa la Wazayuni.
Aliiwasilisha kama eneo la kimbilio la muda kwa Wayahudi kuepusha chuki iliyokuwa inaongezeka huko bara ulaya.
Lakini pendekezo hilo lilikabiliwa na upinzani kutoka vuguvugu ya Kizayuni na Ukoloni wa Uingereza.
"Kulikuwa na mtu anaitwa Boulfor, aliweka kitu kinaitwa maamuzi ya Boulfor na yule jamaa alikuwa anaongelea Uganda kama makazi ya Wayahudi," rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema katika hotuba yake mwaka wa 2016, wakati waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alifanya ziara rasmi Uganda.
"Unaona hawa wenzetu wana mchezo. Kwa bahati mzuri viongozi wa Wayahudi walikataa dhana hiyo," aliongezea.
Lakini kwa nini Uingereza ilitaka Israeli iwe Afrika?
Kulikuwa na hamu ya kudhibiti wimbi la wakimbizi wa Kiyahudi nchini Uingereza baada ya ghasia kali zilizochochewa kwa lengo la kuua au kufukuza kikundi cha Wayahudi Ulaya Mashariki.
Reli ya Uganda iliyojengwa kwa pesa za walipa kodi wa Uingereza zilihitajika kuleta faida kwenye uwekezaji na kupunguza nakisi, na Wazayuni wangeweza kuleta pesa na watu kwenye ulinzi.
Kupata uungwaji mkono wa Kiyahudi kulionekana kuwa muhimu kwa sera za Uingereza baada ya vita vya Boer nchini Afrika Kusini.
Kulikuwa na hangaiko la kweli kwa ajili ya ustawi wa Wayahudi katika Ulaya Mashariki Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Muungano wa Mataifa uliipa Uingereza mamlaka ya kusimamia Palestina.
Lengo lilikuwa kutafuta makazi ya kitaifa ya wayahudi na pia kulinda haki za Waarabu walio wengi.
Mnamo 1947, Umoja wa Mataifa ulipendekeza kugawanywa kwa Palestina katika mataifa tofauti ya Kiyahudi na Kiarabu.
Lakini tukumbuke muda mrefu kabla ya kuundwa rasmi kwa taifa la Israeli mnamo Mei 1948, wahamiaji wa Kiyahudi walikuwa wakiishi Palestina pamoja na Waarabu na Wakristo.