Na Lulu Sanga
Huenda umeshasikia mengi kuhusu jinamizi linalotishia usalama wa chakula barani Afrika na duniani kwa ujumla. Ni hatari kwa afya ya wanyama na binadamu, haitambuliki kwa macho na huwezi kuihisi kwa harufu.
Hii ni sumukuvu. Ni sumu inayozalishwa na kuvu ama fangasi ambao wanaathiri mazao na kusababisha athari za kiafya kwa binadamu na mifugo.
Mara nyingi sumukuvu huathiri nafaka mfano mahindi, ngano, karanga na mazao yatokanayo na mifugo kama vile maziwa na mayai endapo mnyama amekula chakula kilicho athiriwa na sumukuvu.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, tumeshuhudia madhara makubwa ya sumu kuvu na hata kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha, huku wengine wakibaki na maradhi ya muda mrefu.
Kwa mujibu ya Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa kudhibiti Sumukuvu nchini TANIPAC, tatizo la sumukuvu linasababishwa na kutokufuata kanuni sahihi za kilimo ambapo huanzia katika ngazi ya kulima, kuvuna na kuhifadhi.
Hizi ni njia saba za kudhibiti sumu Kuvu?
Hizi ni njia saba ambazo iwapo zitatumika kwa usahihi, basi zinaweza kupunguza makali ya sumukuvu katika chakula cha binadamu na mifugo katika kipindi chote, kabla na baada ya kuvuna.
TANIPAC inashauri kuwa na mzunguko katika upandaji wa mazao. Kubadili mazao katika shamba husaidia kupunguza makali ya sumukuvu. Kwa mfano, kama ulipanda mahindi msimu mmoja, basi msimu mwengine inashauriwa kubadili na kuweka mazao mengine kama vile kunde au hata viazi. Fanya hivi katika misimu tofauti tofauti.
Kutumia mbegu sahihi ambazo zina uwezo wa kuhimili fangasi inayosababisha sumukuvu katika chakula.
Hakikisha pia unakausha vyema vyombo vyako utakavyotumia kuhifadhi nafaka pale unapoanza shughuli ya mavuno. Epuka unyevunyevu wa aina yeyote kwenye vyombo au kifaa chochote kinachohusika na mavuno.
Watafiti pia wanashauri nafaka ikikomaa ni vyema kuvunwa na kukaushwa kuliko kuacha mazao hayo kukaukia shambani, hii inapunguza hatari ya mazao kushambuliwa na kuvu.
Hatua inayofuata ni kuchambua vyema nafaka, ondoa takataka na zile nafaka zilizo haribika kwani kawaida zinabeba sumu kuvu kwa kiwango kikubwa. Kisha kausha vyema nafaka iwe ni mahindi, karanga au ngano.
Kama ni kipindi cha mvua, hakikisha unaanika na kukausha mara kwa mara kabla yakuweka kwenye vihifadhio. Kumbuka, wataalamu wa kilimo wanashauri nafaka zinazo hifadhiwa zinatakiwa kukaguliwa kila baada ya wiki tatu mpaka nne.
Sumukuvu haionekani kwa macho wala kuhisiwa kwa harufu. Kabla yakutumiwa na binadamu hakikisha nafaka hiyo inasafishwa vyema walau mara mbili au mara tatu ili kuondoa uvundo kama upo, lakini pia kuondoa madawa yanayotumika kuhifadhia nafaka. Kisha kausha tena na hapo itakua tayari kusagwa au kukobolewa kwa matumizi salama.
Wataalamu wa afya wanaonya usiwape wanyama mabaki ya nafaka au maji yaliyotumika kusafisha nafaka iliyoathiriwa na kuvu. Kwani hii hupelekea sumukuvu kuathiri wanyama na mwishowe sumu hiyo kupatikana kwenye mayai au maziwa ambayo huathiri zaidi afya ya binadamu.
Baada ya hapo, hakikisha unatunza vyema unga wako unapokua nyumbani. Epuka kuweka nafaka yoyote ile sakafuni kwani ni rahisi kupata unyevunyevu na hivyo kutengeza mazingira rafiki ya kushamiri kwa kuvu.
Tatizo la sumukuvu si geni kwa nchi za Afrika na hata bara la ulaya kwa ujumla. Iliripotiwa awali miaka ya 1950 kwenda 1960 ambapo mifugo mingi ilikufa nchini Uingereza kutokana na karanga ambazo inasemekana asili yake ilikua ni Kusini mwa Marekani.
Mwaka 2005, Kenya iliripoti juu ya vifo vya takriban watu 125 wakati mwaka 2016 Tanzania iliripoti vifo 14 vilivyotokana na sumukuvu.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Chakula ya Kimataifa (IFPRI), kwa wastani, takribani waafrika elfu 26 wanafariki kwa saratani ya ini kila mwaka inayosababishwa na sumukuvu.
Hivyo, jamii inaaswa kuchukua kila tahadhari ya kupambana na sumu hiyo ili kuokoa maisha ya binadamu na mifugo.