Rais Yoweri Museveni wa Uganda anasema Uganda iko tayari kuhusika katika mchakato wa kiafrika wa kusaidia Ukraine na Urusi kumaliza mzozo

Uganda inasema itaunga mkono juhudi za kumaliza mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

Mzozo ulioanza Februari 2022 tangu wakati huo umekuwa na athari nyingi ulimwenguni ikiwa ni pamoja na usambazaji wa chakula kupungua barani Afrika.

Uganda ni kati kundi la nchi za Kiafrika ambazo zinasema zinataka kuunga mkono "mazungumzo ya maana " ambayo yatamaliza mzozo wa urusi na Ukraine.

"Vita hivi vinatuathiri sisi sote na inaweza kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo sasa. Inatishia amani ya ulimwengu. Kwa kuwa tuna mtazamo wetu wenyewe, tunaweza kushiriki nao jinsi tumetatua matatizo yetu wenyewe hapa,” rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema wakati wa mkutano na marais wengine siku ya Jumatatu.

Mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa na rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, pia ulihudhuriwa na rais Azali Assoumani wa Muungano wa Comoros, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

Rais Macky Sall wa Senegal, Abdel Fattah el-Sisi wa Misri, Denis Sassou Nguesso wa Congo Brazzaville na Hakainde Hichilema wa Zambia pia walishiriki.

"Tunahitaji kuthibitisha kwamba tunaanzisha misheni hii kama viongozi wa Pan African, na tunatamani amani," rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema.

Viongozi hao bado hawajaeleza jinsi watakavyotekeleza mazungumzo yao kati ya nchi hizo.

Afrika imesalia kugawanyika kuhusu mzozo huo huku baadhi wakiunga mkono Urusi au Ukraine kwenye kura tofauti katika Umoja wa Mataifa, na wengine wakichagua kutopiga kura.

TRT Afrika