Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno ametangaza kuondoka kwa vikosi vya Ufaransa kutoka nchi hiyo ya Kati mwa Afrika kufikia tarehe 31 Januari.
"Nimeridhishwa na hatua ya kuondoka kwa vikosi vya kwanza vya Ufaransa vilivyokuwa nchini Chad. Wanajeshi wengine watafuata ... hadi vikosi vyote viondoke Januari 31, 2025," Deby alisema katika hotuba yake kwa njia ya Televisheni Jumanne usiku.
Alisema anaamini kuwa uamuzi huo ulikuwa ni matokeo ya "dhamira ya pamoja na halali" ya raia wa Chad."Mapambano yoyote ya uhuru au mamlaka ya nchi yanahitaji kujitolea na kwa hili ilikuwa lazima lifanyike kwa ajili ya vizazi vijavyo, kama wazee wetu walivyojitolea, na kutuachia taifa imara," rais wa Chad alisema.
Mwezi Novemba, Chad ilitangaza ukomo wa makubaliano katika ushirikiano wa masuala ya usalama na ulinzi na Ufaransa kabla ya baadhi ya wanajeshi wa Ufaransa kuanza kuondoka katika nchi hiyo ya kati mwa Afrika Disemba 10.