Na Sylvia Chebet
Um Adel, mkimbizi wa Sudan katika kambi ya Metche mashariki mwa Chad, hajaonana na mume wake kwa zaidi ya mwaka mmoja.
"Amepotea, na sijui yuko wapi," anasema. “Mtoto wetu Khalid alikuwa sawa hadi chakula kilipungua, baada ya siku moja au mbili bila kula vizuri, alikuwa na homa kali, sijisikii vizuri hapa, na hali sio nzuri...nataka kurudi Sudan."
Mwaka Mpya unapoingia, Um Adel anatumai kuwa hali ya kawaida itarejea katika nchi yake, iliyoharibiwa na mapigano kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo.
Mzozo wa ndani nchini Sudan ulizuka Aprili 15, 2023. Takriban watu 60,000 wamepoteza maisha yao tangu wakati huo. Idadi ya waliokimbia makazi yao inazidi milioni 14. Takriban watu milioni 26 wanakabiliana na uhaba mkubwa wa chakula.
Kwa vyovyote vile, Sudan ndiyo janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani. Bado, 2024 ilipita na ulimwengu haukutambua na kuangazia vita vya maeneo mengine, kama vile Israeli-Palestine na Urusi-Ukraine, ziligonga vichwa vya habari.
Mamilioni ya wasio na makazi
Zaidi ya Wasudan milioni 3.2 wamevuka mpaka na kuingia katika nchi jirani za Chad, Sudan Kusini, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri na hivi karibuni Ulaya na Mashariki ya Kati.
Kilichoanza kama mapigano mjini Khartoum sasa ni msururu wa mashambulizi ya anga, milipuko mikubwa ya risasi na milio ya risasi inayoendelea nchini kote kwa muda wa miezi 20.
Kulingana na Umoja wa Mataifa na mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu, mzozo huo umegubikwa na ukatili, ikiwa ni pamoja na mauaji yanayochochewa na kabila na ubakaji.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inachunguza madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Hakuna chakula cha kutosha au maji safi. Watoto wana utapiamlo mkali. Magonjwa yanaenea. Hospitali ziko mbali na si salama. Msaada unacheleweshwa.
"Mgogoro huu mkubwa - mgogoro wa haki za binadamu, mgogoro wa mahitaji ya kibinadamu - unapita kwa kiasi kikubwa bila kuzingatiwa katika jumuiya yetu ya kimataifa," anasema Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi, Filippo Grandi.
Anaamini kwamba hata kabla ya mauaji ya kimbari ya Gaza na Israeli kupewa kipao mbele, vita vya Sudan vilikuwa "vimetengwa" licha ya athari zake kubwa.
Grandi analaani "upungufu wa maslahi katika mizozo barani Afrika", kama ile ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sahel, kama "ya kutisha na ya kushangaza".
Anjiuliza vipi itakuwa taswira ya Sudan hata kama mapigano yatakoma hivi karibuni.
"Ni nini mustakabali wa nchi kama Sudan, iliyoharibiwa na vita?" Grandi anauliza, akiwa na wasiwasi kwamba tabaka la kati la Sudan ambalo "lilishikilia nchi pamoja" limeharibiwa kabisa.
"Wanajua yameisha. Wamepoteza kazi, nyumba zao zimeharibiwa, na wote wameona wanafamilia na jamaa zao wakiuawa. Ni ukatili," analalamika.
Maumivu ya njaa
Uharibifu wa huduma za afya
Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), wamewatibu zaidi ya watoto 40,000 wenye utapiamlo kote nchini Sudan.
Shirika la kimataifa lilianzisha vituo vya kulisha wagonjwa wa kulazwa katika kambi ya Zamzam ya Darfur Kaskazini, El Geneina ya Darfur, Nyala na Rokero, na mashariki mwa Chad, ambako wakimbizi wengi wanaishi.
"Watoto wanakufa kutokana na utapiamlo nchini kote Sudan. Msaada wanaohitaji kwa haraka sana haujafika, na unapofika, mara nyingi unazuiwa," anasema mratibu wa dharura wa MSF huko Darfur.
"Mnamo Julai, kwa mfano, malori yenye vifaa vya MSF yalizuiwa kufika maeneo yao huko Darfur. RSF ilishikilia malori mawili, na watu wasiojulikana wenye silaha walikamata moja."
Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha kuwa mzozo huo umesababisha karibu 80% ya vituo vya afya kukosa huduma, na kulemaza mfumo wa afya ambao tayari unatatizika.
Vifaa vimezuiliwa
Huko El Fasher pekee, vituo vinavyoungwa mkono na MSF vilishambuliwa mara 12, na ni hospitali moja tu ya umma inayofanya kazi kwa kiasi iliweza kufanya upasuaji tangu mapigano yalipoongezeka katika jiji hilo mwezi Mei.
"MSF inajaribu kujaza baadhi ya mapengo. Katika maeneo mengi, sisi ndio shirika pekee la kimataifa linalofanya kazi. Hatuwezi kukabiliana na mgogoro huu mkubwa peke yetu. Tunajitahidi kupata vifaa na wafanyakazi kwa miradi yetu," anasema Esperanza Santos, mratibu wa kushghulukia masuala ya dharura wa MSF Port Sudan.
"Jibu la maana na misaada inayowafikia watu wanaoihitaji zaidi lazima ianze sasa. Hakuna muda zaidi wa kupoteza."
Kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya malaria na magonjwa yanayosambazwa na maji, huku milipuko ya kipindupindu sasa ikitangazwa rasmi katika angalau majimbo matatu.
Tishio la magonjwa yanayozuilika kwa chanjo miongoni mwa watoto, kama vile surua, linakaribia, huku vita hivyo vikiweka kampeni za chanjo kusitishwa. Hali si nzuri zaidi katika nchi jirani ambazo maelfu ya Wasudan wamekimbilia.
Huku maisha, kaya na mustakabali wa nchi ukiwa hatarini, jambo moja ambalo mamilioni ya watu wanaoteseka wanang'ang'ania ni ahadi ya chanya ambayo huja na mwaka mpya.