" Hakuna suluhisho la kijeshi linalokubalika katika mzozo huu".
Hii ndiyo kauli ambayo mamlaka ya serikali ya Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki, IGAD, imesema katika taarifa yake kuelezea matokeo ya mazungumzo kati ya Jeshi la Sudan na Kikundi cha Rapid Support Forces yaliyofanyika Jeddah, Saudi Arabia.
Vita kati ya pande hizo mbili zimeendelea tangu Aprili 15 mwaka huu.
Mazungumzo hayo yalifadhiliwa na ufalme wa Saudi Arabia, Marekani na mamlaka ya IGAD ambayo inajumuisha nchi saba, ikiwemo Sudan.
"Wafadhili wanasikitika kwamba wahusika hawakuweza kukubaliana kuhusu mipango ya utekelezaji wa usitishaji mapigano," taarifa ya IGAD ilisema.
Lakini hii inamanisha nini?
Jeshi la Sudan na Kikundi cha Rapid Support Forces kukosa kukubaliana kusitisha vita kunamaanisha hali ya kibinadamu itaendelea kuzorota huku mapigano yakiendelea.
Tayari Shirika la Madakitari la MSF linaripoti kuwa wakimbizi wanaendeleo kumimika katika nchi jirani ya Chad.
"Kufuatia kuongezeka kwa mapigano huko El Geneina, Darfur Magharibi mwa Sudan, wahudumu wa Médecins Sans Frontières / na Madaktari wasio na Mipaka (MSF) wanaofanya kazi mpakani mashariki mwa Chad wameona ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaowasili katika eneo hilo," Shirika hilo limesema katika taarifa yake.
Chad ni nchi jirani ya Sudan na imekuwa ikipokea wakimbizi kwa wingi, ikiwa wengine wanakimbilia Sudan Kusini, Ethiopia na Misri.
Takriban watu 450,000 wanapata hifadhi nchini Chad tangu Aprili, na idadi hii mbali na ile ya ambao tayari wamekimbia makaazi yao kutoka Sudan na nchi nyingine.
Licha ya kuwa moja ya nchi maskini zaidi na kukabiliwa na changamoto kubwa za kibinadamu, Chad inahifadhi karibu wakimbizi milioni.
"Katika siku tatu za kwanza za mwezi wa Novemba, tuliona wakimbizi wengi wapya waliofika kutoka Sudan kuliko wakati wa mwezi mzima uliopita, takriban watu 7,000 walivuka mpaka," anaelezea Stephanie Hoffmann, mratibu wa uhamasishaji wa MSF huko Adré, mji wa Chad kwenye mpaka na Sudan.
"Tumeona wanawake na watoto ambao walilazimika kuondoka Sudan bila chochote, kwani nyumba zao zilikuwa zikiharibiwa," Hoffman anaongezea.
Shirika hilo linasema lilipokea watu 36 waliojeruhiwa mwishoni mwa wiki.
Makazi yanageuka makaburi
Umoja wa Mataifa unasema ndani ya Sudan, watu milioni 4.5 wamekimbia makazi yao tangu Aprili, wakati vita vilipoanza, wakati wengine milioni 1.2 - wengi wao wakiwa wanawake na wasichana - walikimbilia nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Chad.
"Vita vilivyozuka ghafla vilibadilisha nyumba za Sudan zilizokuwa na amani hapo awali kuwa makaburi," alisema Dominique Hyde, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Nje wa Shirika la Kutetea Wakimbizi, UNHCR.
"Mbali na macho ya ulimwengu na vyombo vya habari, mzozo nchini Sudan unaendelea kupamba moto. Kote nchini, mzozo wa kibinadamu usiofikirika unaendelea, huku watu wengi zaidi wakihama makaazi yao kutokana na mapigano hayo yasiyoisha,” aliongeza Hyde.
Shirika na jamii za kimataifa zimeomba pande hizo mbili angalau kuheshimu azimio lao la kukubali mahitaji ya kibinadamu kuwafikia wananchi katika maeneo yalioathiriwa.
Ikiwa Umoja wa Mataifa unasema takriban watu milioni 25 - wanahitaji msaada wa kibinadamu huku uhamiaji wa ndani, magonjwa na unyanyasaji wa kijinsia vikikithiri.