Rais wa Sudan Abdel-Fattah Al-Burhan akihutubia kikao cha 78 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa UNGA Mjini New York, Marekani, Septemba 21, 2023. Picha: REUTERS / Eduardo Munoz

Jenerali Abdel-Fattah Al-Burhan amesema kuwa hamu yake ilikuwa kutafuta suluhu kudumu ya amani kwa mgogoro unaoendelea nchini Sudan ambao mpaka sasa umesababisha vifo vya vya maelfu ya raia huku mamilioni wakihama makazi yao.

Al-Burhan amefanya ziara kadhaa za kigeni katika wiki za hivi karibuni baada ya kutotoka Sudan kwa miezi ya kwanza ya vita. Amefafanua kuwa amekusudia kutafuta suluhu, wala sio kuomba msaada wa kijeshi, ingawa awali alitaka baadhi ya majimbo kuzuia kupokea misaada nje ambayo anadai RSF inapokea.

Mkuu huyo wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan ameongeza kuwa ameyataka majimbo jirani kuacha kutuma askari wa mamluki kuwaunga mkono vikosi vya Msaada wa Haraka wa Kijeshi (RSF).

"Tuliwaomba majirani zetu kutusaidia kupiga doria mipakani ili kuzuia mtiririko wa askari wa kulipwa na mamluki," alisema Al-Burhan.

Vita livitokea kati ya Jeshi la Sudan SAF na RSF katikati ya mwezi Aprili kufuatia mipango ya mpito wa kisiasa na ujumuishaji wa RSF katika jeshi la Sudan, miaka minne baada ya kiongozi wa muda mrefu Omar Al-Bashir kupinduliwa kupitia uasi wa watu.

Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu Hemedti, anasema tayari kusitisha mapigano na kufanya mazungumzo ya kisiasa. Picha: Reuters 

Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, katika mahojiano, pia ameiambia Reuters kwamba anapendelea kuwepo kwa makubaliano ya mazungumzo kama njia ya kukomesha vita hivyo.

"Kila vita huishia amani, iwe ni kupitia mazungumzo au nguvu. Tunaendelea na njia hizo mbili, na njia tunayopendelea ni njia ya mazungumzo," Al-Burhan alisema kando ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA, huko New York nchini Marekani.

Kiongozi huyo pia ameongeza kusema kuwa anaamini mazungumzo yaliyositishwa na Saudi Arabia na Marekani huko Jeddah bado yanaweza kufanikiwa.

Kwa upande mwingine, kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti, alisema katika ujumbe wa video uliotolewa siku ya Alhamisi na kuambatana na hotuba ya Al-Burhan katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba alikuwa tayari kusitisha mapigano na kufanya mazungumzo ya kisiasa.

Hii sio mara ya kwanza kwa viongozi hao kuonyesha nia ya kusitisha mapigano kwa njia ya mazungumzo, hata hivyo utekelezaji wake ndio umekuwa kizungumkuti.

Reuters