Mkuu wa jeshi la Sudan ameonya kuwa vita nchini humo vinaweza kusambaa katika eneo hilo huku akitoa wito kwa shinikizo la kimataifa kwa kitengo cha kijeshi anachopigana nacho.
Akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan aligusia uhusiano wa wapinzani wa Rapid Support Forces, RSF, na Wagner, kundi la mamluki la Urusi lililokumbwa na vikwazo vya Magharibi kutokana na madai ya unyanyasaji barani Afrika.
Al-Burhan ndiye mtawala mkuu, na kiongozi anayetambulika kwa sasa, wa Sudan tangu mapinduzi ya 2021.
Mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya takriban watu 7,500, na kuwafanya watu wapatao milioni tano kuyahama makazi yao, na kusababisha pigo kubwa kwa juhudi za kuleta demokrasia nchini Sudan.
Takriban milioni moja ya waliokimbia makazi yao walikimbilia nchi jirani.
"Hatari ya vita hivi sasa ni tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa kwani waasi hao wameomba kuungwa mkono na wapiganaji wa sheria na makundi ya kigaidi kutoka mataifa tofauti katika eneo na dunia," Burhan alisema.
"Hii ni kama cheche za vita, vita ambavyo vitaenea hadi nchi nyingine katika kanda," alisema.
"Uingiliaji wa kikanda na kimataifa wa kusaidia makundi haya uko wazi kwa sasa. Hii ina maana kwamba hii ni cheche ya kwanza ambayo itateketeza eneo hilo, na itakuwa na athari za moja kwa moja kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa."
Kikundi cha kigaidi
Vita vilianza Aprili 15 baada ya kusambaratika kwa mpango wa kuunganisha jeshi na Vikosi vya Rapid support Forces , vinavyoongozwa na naibu wa zamani wa Burhan, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.
Burhan amezidi kuzunguka ulimwengu katika wiki za hivi karibuni katika kile kinachoonekana kama juhudi za kutetea uhalali wake.
Katika kikao cha Umoja wa Mataifa, alihimiza mataifa yenye nguvu duniani kutaja Vikosi vya Msaada wa Haraka, au RSF, kama kundi la kigaidi.
"Wamefanya kila aina ya uhalifu unaotoa sababu za kuteuliwa," alisema.
"Wale ambao wameunga mkono mauaji, uchomaji moto, ubakaji, uhamisho wa lazima, uporaji, wizi, utesaji, usafirishaji wa silaha na dawa za kulevya, kuleta mamluki au kuandikisha watoto - uhalifu wote kama huo unahitaji uwajibikaji na adhabu," alisema.
Mpinzani wa Burhan aongea
Marekani mapema mwezi huu iliweka vikwazo kwa viongozi wa RSF akiwemo kamanda mkuu Abdelrahim Hamdan Daglo, kaka wa kiongozi wa kundi hilo, kutokana na madai ya dhuluma ikiwa ni pamoja na mauaji ya gavana wa Darfur Magharibi.
Lakini Marekani na nchi zingine za Magharibi pia zimekuwa zikimkosoa vikali Burhan.
Pamoja na kiongozi wa RSF Daglo, Burhan mwaka 2021 aliuweka pembeni uongozi wa kiraia ambao ulikuwa sehemu ya makubaliano ya mpito ya kugawana madaraka kufuatia maandamano makubwa yaliyomuangusha dikteta wa muda mrefu Omar al-Bashir.
"Bado tunajitolea kwa ahadi zetu za awali za kukabidhi madaraka kwa watu wa Sudan kwa maridhiano na ridhaa kubwa ya kitaifa," alisema. "Majeshi ya kijeshi yangeacha siasa mara moja na kwa wote."
Kusitisha vita
Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kwa jina la Hemedti, alisema katika ujumbe wake wa video kwamba vikosi vyake viko tayari kikamilifu kwa usitishaji mapigano na mazungumzo ya kina ya kisiasa ili kumaliza mzozo huo.
Mawasiliano mengi ya hivi karibuni ya Hemedti yamekuwa ni ujumbe wa sauti, na mahali alipo kumekuwa chanzo cha uvumi.
Katika video hiyo iliyotolewa siku ya Alhamisi muda mfupi kabla ya Burhan kuzungumza, Hemedti alionekana akiwa amevalia sare za kijeshi, akiwa ameketi nyuma ya meza na bendera ya taifa la Sudan nyuma yake alipokuwa akisoma hotuba yake. Mahali alipo hapakuwa wazi.
"Leo tunasisitiza upya ahadi yetu ya mchakato wa amani wa kusimamisha vita hivi," Hemedti alisema. "RSF imejiandaa kikamilifu kwa kusitisha mapigano kote nchini Sudan ili kuruhusu kupitishwa kwa misaada ya kibinadamu ... na kuanza mazungumzo mazito na ya kina ya kisiasa."