Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amekutana na rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye. Picha: Ikulu ya Burundi

Rais Hassan Sheikh Mohamud ambaye amekuwa Burundi kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, walijadili kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo na mwenyeji wake Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi.

Wawili hao waliwaongoza wawakilishi wa serikali hizo mbili ambapo waliangazia masuala yaliyoambatana na hali ya usalama nchini Somalia na ukanda kwa jumla.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amemuandalia Rais Sheikh na ujumbe wake karamu ya heshima.

Katika mkutano wao, viongozi hao wawili waligusia hitaji la haraka la kusitisha mapigano nchini Sudan mara moja ili kuruhusu msaada wa kibinadamu na kupata suluhisho la kudumu kwa mzozo nchini humo kupitia mazungumzo ya amani.

Rais Hassan Sheikh alipongeza juhudi za serikali ya Burundi ya kudumisha amani na usalama, hasa kupitia mchango wa vikosi vya Burundi katika ujumbe wa mpito wa vikosi vya Afrika nchini Somalia (ATMIS).

Viongozi hao wawili wamewaagiza Mawaziri wao wa Mambo ya Nje kushirikiana kuandaa kikao cha tume ya Pamoja ya kudumu ya Ushirikiano (JPCC), ambayo inakusudia kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya raia wa pande zote mbili.

TRT Afrika