Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametia saini muswada kuwa sheria siku ya Jumanne ambao utabadilisha hukumu ya wafungwa 60 wanaosubiri kunyongwa na kuwa kifungo cha jela / Picha: AP

Zimbabwe imefuta rasmi hukumu ya kifo baada ya Rais Emmerson Mnangagwa kutia saini mswada kuwa sheria siku ya Jumanne, na badala yake kubadilisha hukumu ya wafungwa 60 wanaosubiri kunyongwa, kuwa kifungo cha jela.

"Haya siyo tu maendeleo makubwa kwa Zimbabwe, pia ni mwanga wa matumaini kwa vuguvugu la kukomesha uasi katika kanda, na hatua kubwa katika harakati za pamoja za kimataifa za kukomesha adhabu hii ya kikatili, ya kinyama na ya kudhalilisha," Lucia Masuka, mkurugenzi mkuu wa shirika la Amnesty international amesema.

Unyongaji wa mwisho ulifanyika karibu miongo miwili iliyopita mnamo 2005, kwa sababu wakati fulani hakuna mtu ambaye alikuwa tayari kuchukua kazi ya kuwa mnyongaji wa serikali.

Rais Mnangagwa alikabiliwa na hukumu ya kifo mwenyewe katika miaka ya 1960 wakati wa vita vya uhuru wa Zimbabwe.

Kabla ya kusainiwa kwa muswada huo, sheria husika ya Zimbabwe iliruhusu hukumu ya kifo katika kesi za mauaji yaliyofanywa chini ya hali mbaya.

Kifungu kipya katika Sheria ya Ulinzi kilichoanzishwa na Sheria ya Kukomesha Adhabu ya Kifo, 2024 kinaruhusu kurejeshwa kwa adhabu ya kifo wakati hali yoyote ya hatari ya umma inatangazwa kwa mujibu wa kifungu cha 113 cha Katiba.

Kufikia leo, nchi 24 za Afrika zimekomesha kikamilifu hukumu ya kifo, ikiwa ni pamoja na Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sierra Leone na Zambia - ambazo zilifanya hivyo tangu 2020.

Hadi sasa nchi 113 zimekomesha kabisa hukumu ya kunyongwa.

TRT Afrika