Precious Marange alikuwa akifanya kazi kama msaidizi wa nyumbani nchini Zimbabwe, alipoona mchezo wa kriketi kwa mara ya kwanza kwenye televisheni ya mwajiri wake.
Mchezo huo unaochezwa na wachezaji 22 na wenye mwendo wa kasi na wa kusisimua, ulimshangaza Precious.
Wiki chache baadaye, fursa ya kushiriki katika mechi ya kriketi katika mji mkuu wa Zimbabwe wa Harare ilijitokeza. Precious alichukua fursa hio na kuwa mchezaji wa kriketi hadi leo.
"Nilipitia Klabu ya Kriketi ya Takashinga mwaka wa 2004 wakati nilihisi hamu ya ghafla ya kujaribu mchezo huo," anaisimulia TRT Afrika. "Makocha walinipa fursa, na nimekuwa nikicheza tangu wakati huo."
Takashinga ni miongoni mwa vilabu vya kwanza vya kriketi nchini Zimbabwe yenye wachezaji weusi na chimbuko la wachezaji wengi bora.
Precious mara nyingi alikuwa akitoroka kwenda kwenye klabu kufanya mazoezi kabla ya kukimbia kuwahi kwenye kazi zake za nyumbani katika kitongoji cha Highfield cha Harare.
"Fursa yangu kubwa ya kwanza ilikuja mwaka wa 2006 nilipopata nafasi ya kusafiri na timu ya kriketi hadi Botswana na pia kucheza katika mechi ya kuwania ligi ya Afrika mwaka huo huo," mchezaji huyo anakumbuka. "Nilipanda ndege yangu ya kwanza kuelekea Afrika Kusini katika mechi dhidi ya Pakistan mwaka 2008."
Mwanariadha mahiri
Mwenzake alipopendekeza Precious ajaribu raga pia, hangeweza kufikiria kufanya vyema katika mchezo mwengine mpya na baada ya kuujaribu mchezo huo alifaulu na kupata kufikia hadhi ya mwanariadha bora.
"Lazima nidumishe kiwango fulani cha ubora kila wakati ili kucheza kriketi na raga," anaeleza.
"Ninahifadhi umbo langu kupitia mazoezi ya kuongeza nguvu na mazoezi ya viungo vya kuongeza hewa ili kuboresha kasi yangu, wepesi, na nguvu uwanjani."
Nidhamu yake na maadili ya kazi vilimuwezesha Precious sio tu kuchezea nchi yake kriketi na raga bali pia nahodha wa timu za taifa katika michezo yote miwili.
Utaratibu wa kila siku wa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 41 unaanza na mazoezi saa kumi na moja asubuhi kabla ya kuanza kazi yake katika kiwanda cha chuma saa moja na nusu asubuhi.
Licha ya kupata mafanikio ya kitaifa katika raga na kriketi, Precious anathamini kazi yake ya kiwandani kwani inamsaidia kumpatia mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 12 na watu wengine wa familia yake wa karibu maisha bora.
"Napata muda wa mchezo na kushughulikia famili yangu. Mtoto wangu anafurahi sana akijua mama yake atafanya lolote lile kuhakikisha anapata maisha bora," anasema Precious, ambaye huwasaidia wanafamilia wengine watano.
"Nahakikisha watu wote wako sawa, ingawaje pesa hazitoshi."
Mfano wa kuigwa
Precious anawashukuru waajiri wake na wakuu wa kiwanda hicho, ambao wamekuwa wakimuunga mkono kwa kumruhusu mara kwa mara kuchukua likizo ili kuendelea na kazi yake ya michezo.
"Wakubwa wangu ni kama wazazi wangu. Wananiunga mkono kwa kila kitu. Wanaelewa heshima ya kuwakilisha Zimbabwe katika raga na kriketi," anaiambia TRT Afrika.
Huku michezo ya wanawake nchini Zimbabwe ikipata umaarufu, mafanikio ya Precious yanaonekana kuwatia moyo wengine wengi kujaribu kujipenyeza katika viwanja vinavyotawaliwa na wanariadha wa kiume hadi sasa.
Akiwa mmoja wa wachezaji waandamizi katika timu zote mbili, Precious anachukuliwa kuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wachanga wanaotamani mafanikio ya kimataifa.
Lengo lake kuu ni kuanzisha chuo cha michezo ambapo wanawake wa rika tofauti na wa asili tofauti watapata fursa ya kufanya vyema katika mchezo wao waliouchagua.
"Kila mwanamke anaweza kucheza michezo iliyotawaliwa na wanaume," anasema Precious. "Umri ni nambari tu, na hakuna kisichowezekana."