Raia wa Sudan wanaokimbia migogoro ya ndani wanavumilia hali mbaya katika kambi za wakimbizi, wakipambana na hali ya hewa ya baridi na mzozo wa chakula.
Picha iliyotolewa na shirika la habari la Anadolu inaangazia masaibu ya watu waliohamishwa makazi yao katika Kambi ya Goz al-Haj, ambapo maelfu wanasimulia matukio ya kuhuzunisha na mapambano yao yanayoendelea ya kuokoa maisha.
Kambi hiyo iliyoko mji wa Shendi, kaskazini mwa mji mkuu Khartoum, imekuwa makazi ya karibu wakimbizi 8,000 wa Sudan kwa muda wa miezi miwili iliyopita.
Kambi hiyo inajumuisha takriban mahema 300 ambapo wakaazi wanakabiliwa na uhaba wa chakula, hali mbaya ya hewa, na usaidizi duni wa huduma za afya.
Mfamasia Fawwaz Abdulbaki, ambaye alitafuta hifadhi katika kambi hiyo, alielezea maisha katika kambi hiyo.
'Maisha ya jahanamu' "Baada ya RSF (Vikosi vya Msaada wa Haraka) kuingia kijijini kwetu, ilikuwa ni kama kuishi kwenye jahanamu," Abdulbaki alisema.
Aliongeza kuwa RSF iliwachukulia kama si binadamu. "Tuliacha kila kitu nyuma - nyumba zetu, pesa zetu - na kukimbia bila chochote. Sasa, tunachotaka ni kurejea majumbani mwetu," Abdulbaki alisema zaidi.
Pia alielezea changamoto zilizopo katika kambi hiyo, ikiwa ni pamoja na uhaba wa chakula na blanketi.
"Ingawa baadhi ya mashirika ya kibinadamu na wafadhili wanatoa misaada, haitoshi. Ombi langu kwa mashirika ya kimataifa: tusaidie. Watu hapa wanateseka," aliongeza.
Khalid Mohammed Jaafar, mwalimu anayeishi katika kambi hiyo, alisimulia jinsi vikosi vya RSF vilivyojipenyeza katika jamii yake, na kusababisha mateso makubwa.
Wanamgambo walitaka dhahabu
"Waliishi majumbani mwetu, wakatupiga, na kutaka dhahabu, silaha, na simu za rununu. Na hata kuvunja heshima yetu," Jaafar alisema.
Ili kutoroka, Jaafar na wanakijiji walianza safari ngumu alfajiri, wakitembea kwa kilometa na watoto, wazee, na wagonjwa chini ya hali mbaya.
“Njiani wanawake walijifungua chini ya miti, miguu ya watoto ilivimba na wachache walifariki baada ya kufika kambini, hata mama yangu alifariki kutokana na hali ngumu njiani na masafa marefu,” alisema Jaafar.
Akieleza kuwa wanahangaika na uhaba wa chakula, baridi na magonjwa katika kambi hiyo, Jafaar aliongeza kuwa kung'atwa na nge na nyoka ni tishio kubwa na kwamba ndugu zake wawili wamekufa kwa kuumwa na nyoka siku chache zilizopita.
Ravda al-Tayyeb, mkazi mwingine wa kambi hiyo, alizungumza kuhusu uamuzi wa wanakijiji kuondoka: "Wanaume wetu hawakuondoka kwa kuhofia maisha yao bali kulinda heshima yao. Hakuna anayeweza kusimama na kutazama utu wao ukidhalilishwa."
Hali mbaya
Tangu Aprili 2023, Sudan imekumbwa na mzozo kati ya jeshi na RSF, unaotokana na mizozo kuhusu mageuzi ya kijeshi na ushirikiano wa mamlaka.
Mapigano yanayoendelea yameharibu miundombinu ya taifa, uchumi, elimu, na mifumo ya afya.
Juhudi za kupatanisha na kuleta amani zimefeli, na kuwaacha mamilioni ya watu katika hali mbaya.
Kulingana na UN, zaidi ya watu 20,000 wamekufa, milioni 3 wamekimbia nchi, na karibu milioni 9 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani.
Zaidi ya watu milioni 25 sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Katika Kambi ya Goz al-Haj, wakaazi wanaendelea kuhangaika ili kuishi maisha ya kawaida, wakiwakilisha hali moja tu ya jamii nyingi zilizoathiriwa na mzozo wa muda mrefu wa Sudan.