Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Tanzania inalenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme nchini humo kufuatia mpango wa kuanza kununua nishati hiyo kutoka Ethiopia.
Tayari, mamlaka za nishati kutoka nchi hizo zipo kwenye meza ya majadiliano kukubaliana kuhusu vifungu, vigezo na masharti ya makubaliano hayo ya miaka 20.
Katika makubaliano hayo, Shirika la Umeme la Ethiopia litakuwa linaiuzia Tanzania nishati ya umeme, kupitia shirika la TANESCO.
Mpango huo, unatarajiwa kuanza baadaye mwaka 2024.
Kwa kuanzia, Tanzania inalenga kununua Megawati 100 za umeme kutoka Ethiopia, baada ya kukamilika kwa majadiliano ya awali.
"Lengo la mpango huu ni kuunganisha mradi wa umeme wa Afrika Mashariki na ule wa Kusini mwa Afrika, ambapo Tanzania itakuwa katikati ya miradi hiyo miwili. Kukamilika kwa huu mpango huu, kutafanikisha kuuziana umeme kati ya nchi za Afrika Mashariki na zile za Kusini mwa Afrika," anaeleza Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, kutoka Wizara ya Nishati nchini Tanzania.
Hata hivyo, ili mradi huo ukamilike, ni muhimu kwa mikataba kadhaa ipitiwe kati ya Tanzania na Kenya.
"Mambo yote hayo yapo kwenye hatua za majadiliano ambayo hujulikana kitaalamu kama ‘Wheeling Charges Agreement’," amesisitiza Luoga.
Kulingana na Kamishna huyo, makubaliano hayo yakishakamilika, Ethiopia itaanza kuiuzia umeme Tanzania.
Kupitia mradi huo, pia Tanzania itakuwa imejitosheleza katika nishati ya umeme, na hivyo kuwa na uwezo wa kuiuzia tena Ethiopia au nchi yoyote katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Na hata kama Tanzania itakuwa na nishati ya ziada kabisa, basi tutaweza hata kuuza umeme wetu hadi Afrika Kusini," anaiambia TRT Afrika katika mahojiano maalumu.
Hali kadhalika, Tanzania inalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa yake ya kanda ya Kaskazini, ambayo inahusisha Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara, ikishakamilisha mpango wa ununuzi wa umeme kutoka Ethiopia.
Kamishna Luoga anasema kuwa kanda hiyo inakabiliwa na mahitaji makubwa ya nishati ya umeme, ukilinganisha na kiwango cha uzalishaji cha sasa.
"Mahitaji ni makubwa sana kule tofauti na uzalishaji, kwahiyo kwa kuchukua umeme Ethiopia Megawati 100, kutaenda kuimarisha upatikanaji wa umeme katika kanda hiyo ya kaskazini," anaeleza.
Kamishna huyo Umeme na Nishati Jadidifu anasema kuwa umeme huo utapitia Kenya ukitokea nchini Ethiopia, mpaka kituo cha Lemugulu, kilichopo katika eneo la Kisongo mkoani Arusha, kabla ya kusambazwa katika kanda zingine zilizobakia.
Mradi wa umeme wa Julius Nyerere
"Mitambo mitatu tayari imeshawashwa, yenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kila mmoja, hivyo kuzalisha jumla ya megawati 705 zinazoingizwa katika gridi ya taifa," alisema Waziri huyo.
Hata hivyo, pamoja na malengo ya mradi huo unaogharimu Dola Bilioni 2.2, mahitaji ya umeme nchini Tanzania yameongezeka kwa asilimia 15.
"Kabla ya mradi wa JNHPP mahitaji ya umeme yalikuwa megawati 1300 tu, ila kufikia Februari 2024, mahitaji yamefikia 1,700 megawati," Luoga anasema.
Luoga anaongeza kwa kusema kuwa kutokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa, mradi wa JNHPP utazidiwa nguvu na hautotosha, pengine ndani ya miaka miwili tu.
"Umeme tunaochukua nje ni wa gharama nafuu zaidi kuliko ule ambao TANESCO anamuuzia mwananchi hapa nchini Tanzania."
Kulingana na Luoga, majadiliano yanaendelea kati ya Shirika la Umeme la Ethiopia na Tanzania, kuona namna gani ya kutekeleza makubaliano hayo ya miaka 20.
"Tuko kwenye meza ya majadiliano, uniti moja ya umeme inaweza kuuzwa kwa Dola 0.7, tofauti na ile ya TANESCO ambayo mwananchi wa kawaida kwa Dola 0.9," anasema.
Si mara ya kwanza
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kununua nishati ya umeme kutoka nje ya nchi.
Kwa mfano, kwa sasa, umeme wa mkoa wa Kagera unatoka nchini Uganda, kwani mkoa huo hauko kwenye Gridi ya Taifa.
Hali kadhalika, mkoa wa Rukwa nao unatoa nishati yake ya umeme kutoka mji wa Mbala ulioko nchi ya jirani ya Zambia, huku nchi hiyo ikiipa Tanzania kiasi cha megawati 12.