Corona Cermak akiwa katika moja ya vipindi vyake vya Kiswahilli katika Chuo Kikuu cha Masaryk cha nchini Chekia. /Picha: Corona Cermak

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Jambo. Habari gani. Nzuri sana.

Hayo ni baadhi tu ya maneno yanayowakilisha salamu kwenye lugha hii adhimu duniani.

Kutambuliwa na UNESCO

Ni miaka mawili sasa, tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutenga Julai 7 ya kila mwaka kama siku ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili.

Mkutano Mkuu wa UNESCO uliofanyika Novemba 23, 2021 uliamua kuwa, siku ya Kiswahili Duniani iadhimishwe kila mwaka.

Kwa sasa, Kiswahili ni lugha ya taifa kwa nchi kadhaa ikiwemo Tanzania, Uganda na Kenya.

Lugha nyingine zinazotambulika duniani ni kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kirusi, Kispanyola na Kiarabu.

Ufahari

"Wazungumzaji wa lugha hiyo adhimu wanapaswa kujisikia fahari, popote pale walipo," Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA), Consolata Mushi anaiambia TRT Afrika.

“Uamuzi huu una maana kubwa sana kwetu wazungumzaji wa Kiswahili, kwani inadhihirisha kuwa hii si lugha ya Afrika pekee, ni lugha inayozidi kuvuka mipaka,” anaeleza.

Mkutano Mkuu wa UNESCO uliofanyika Novemba 23, 2021 uliamua kuwa, siku ya Kiswahili Duniani iadhimishwe kila mwaka./Picha: Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa UNESCO, kwa sasa, idadi ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili inafikia milioni 500, ulimwenguni kote.

“Kwa sasa, kuna vyuo na vituo zaidi ya 150 duniani vinavyotumia lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya mawasiliano,” anasema Katibu Mtendaji huyo wa BAKITA.

Kulingana na Mushi, uwepo wa vyombo mbalimbali vya habari, pia umechangia lugha hii kuvuka mipaka kwa kasi ya ajabu, huku akiweka wazi kuwa kuna vituo vya televisheni na redio zaidi ya 44 vinayotangaza kwa kutumia Kiswahili, vinne kati ya hivyo vikiwa vinapatikana nchini Ethiopia.

Mushi anaongeza kuwa, kati ya nchi nane zinazopatikana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), nne zimeidhinisha Kiswahili kama lugha yao ya taifa.

Wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili toka Jumuiya ya Afrika Mashariki wameendelea kuwaomba wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo kuongeza jitihada za kuiimarisha lugha ya Kiswahili na kubuni mbinu bora za kukuza na kuiendeleza lugha hiyo./Picha: TRT Afrika.

Nchi hizo ni pamoja na Tanzania, Uganda, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Utayari wa Taasisi za Kikanda

Mwaka 2022, Umoja wa Afrika ulipitisha lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya kikazi ndani ya taasisi hiyo yenye nchi wanachama 55.

Bunge la Afrika (PAP) walishafanya hivyo siku nyingi ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), japo EAC walianza kwa kusuasua.

Utajiri wa lugha ya Kiswahili

Lugha hii adhimu duniani imejengwa kwenye misingi ya lahaja.

Kwa ufupi, lahaja ni lugha mbalimbali za pwani zilizokuwa na uhusiano wa karibu sana.

Mahakama ya ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yenye makao makuu yake nchini Tanzania, imekuwa ikitumia lugha ya Kiswahili katika usikilizwaji wa kesi zake./Picha: AfCHPR

Lugha hizo ni kama vile Kiamu, Kimvita, Kijomvu, Kimtang’ata, Kimakunduchi, Kitumbatu, Kimgao, Kiunguja na Ci-mbalazi.

Hata hivyo, tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa Kiswahili kina lahaja 13 hadi 20.

Kiswahili kutoka Kiarabu

Pamoja na kuundwa kwa lahaja tofauti, lugha ya Kiswahili pia imeazima asilimia kati ya 20 hadi 30 ya maneno yake kutoka kwenye lugha ya Kiarabu.

“Hii ilifanyika zaidi wakati wa biashara zilizohusisha watu wa pwani ya Afrika Mashariki na Waarabu, ambapo waarabu wakakuta jamii za ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki wakizungumza lugha yao, na wakawaita ‘Wasahil’,” Katibu Mtendaji wa BAKITA anaeleza.

Kikao cha Umoja wa Afrika./Picha: AU

Hata hivyo, pia yapo maneno kutoka lugha mbali mbali za kimataifa kama vile ‘Mvinyo’ kutoka lugha ya Kireno au ‘Shule’ kutoka lugha ya Kijerumani, na kadhalika.

Nani mmiliki halali wa Kiswahili?

Kwa miaka mingi sasa, kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu ni nchi gani kwenye ukanda wa Afrika Mashariki yenye kuongea lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.

“Kiswahili fasaha na sanifu ni kile kinachozungumzwa nchini Tanzania, na hii ni kwa sababu za kiidhibati. Hata wenzetu Wakenya wanajua hilo. Sina maana kuwa wengine wanazungumza Kiswahili kibovu”.

TRT Afrika