Makao Makuu ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) yaliyoko nchini mjini Abidjan nchini Cote D'Ivoire./Picha: Reuters

Kenya inashika nafasi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kupokea misaada ya maendeleo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), katika kipindi cha miaka 10.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na taasisi hiyo yenye makao makuu yake mjini Abidjan nchini Cote D'Ivoire, Kenya ndiye mnufaika mkubwa wa fedha hizo, ikipokea kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 3.718, fedha ambazo zitatumika kufadhili miradi ya nchi hiyo.

Tanzania inashika nafasi ya pili, ikiwa imepokea Dola za Kimarekani bilioni 2.83, kati ya mwaka 2013 hadi 2023, wakati Rwanda ilipokea kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1.81 kutoka kwa AfDB.

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) hutoa pesa kwa serikali za nchi za Afrika ili kusaidia miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha hali ya maisha ya watu na kujenga uchumi wa nchi.

Hii ni miradi ambayo imeundwa ili kutengeneza ajira, kuboresha upatikanaji wa huduma za msingi, vile vile kutoa huduma bora za afya na elimu.

Mifano ya miradi ya maendeleo ni pamoja na kujenga barabara na madaraja mapya, kusaidia wakulima kuimarisha kilimo, kuboresha hospitali, ujenzi na kadhalika.

Fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika hutokana na vyanzo mbalimbali, ikiwemo usajili wa wanachama wake, riba kutokana na mikopo kwa nchi za Kiafrika, pamoja na fedha zilizokopwa kwenye masoko ya kimataifa.

TRT Afrika