Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amezitaka nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba kutumia kila fursa inayopatikana kuishinikiza Israeli na washirika wake.
Akizungumza kwenye mkutano wa 6 wa GCC mjini Doha mji mkuu wa Qatar siku ya Jumapili , Fidan alisema: “Hali na unyanyasaji wa kikatili unaowakabili wafungwa wa Kipalestina hauwezi kupuuzwa."
"Wacha tuwe karibu kutetea sheria za kimataifa, haki za binadamu, na maadili ya ulimwengu ambayo baadhi ya marafiki zetu wa Magharibi wamesahau," alisema.
"Ushirikiano wetu wa karibu ni wa muhimu sana katika kutafuta amani na usalama katika ukanda wetu, tukianzia na kupata walau suluhu kwa ajili ya ndugu zetu Wapalestina," aliongeza Waziri wa Mambo ya Nje ya Uturuki.
Fidan alisisitiza kuwa Israeli inatekeleza "uhalifu wa kinyama" huko Gaza , na kwamba ukimya wa baadhi ya nchi lazima ukomeshwe.
"Tuko tayari kuchangia ujenzi mpya wa Gaza, lakini wale walioharibu Gaza na kusaidia katika uharibifu wake lazima pia walipe fidia kwa uharibifu huu," alisema.
Fidan alisema kuwa upinzani dhidi ya uhalifu katika eneo la Palestina umeibua mvutano mkubwa kati ya wakandamizaji na wale wanaokandamizwa
"Kutambuliwa kwa Taifa la Palestina na nchi nyingi zaidi na uanachama wake kamili katika Umoja wa Mataifa ni hitaji la sheria ya kimataifa, haki, na lenye dhamiri," alisema.
"Kama Uturuki, tutaendelea kufanya kila juhudi kuanzisha Taifa huru, ne lenye kushikamana kijiografia la Palestina," Fidan aliongeza.
Uhusiano na nchi za Ghuba
Fidan alionyesha imani yake kwamba mkutano huo ungeleta matokeo madhubuti, akisema: "Kama Uturuki, tunatilia maanani sana uhusiano wetu na nchi za Ghuba."
“Hatua tuliyofikia katika mahusiano yetu leo, ni kutokana na juhudi zetu za pamoja, inafurahisha.
Uhusiano wetu unaendelea kuimarika katika kila eneo,” aliongeza.
Fidan alisema kuwa jumla ya biashara kati ya Uturuki na nchi za GCC iliongezeka kwa takriban asilimia 40 mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka uliopita, na kufikia dola bilioni 31.4, na kwamba kiwango cha biashara kimeongezeka mara 16 katika miaka 20 iliyopita.
Alisisitiza kuwa Uturuki ni mojawapo ya vivutio muhimu vya utalii kwa nchi za Ghuba, akibainisha kuwa zaidi ya raia milioni 1.5 wa Ghuba walitembelea nchi hiyo mnamo 2023.
Israeli imeendeleza mashambulizi yake ya kikatili huko Gaza tangu Oktoba 7 kundi la wapiganaji wa Hamas liliposhambuliwa licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Kulingana na mamlaka za afya, zaidi ya Wapalestina 37,000 wameuwawa katika eneo la Gaza, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na karibu watu 84,500 wamejeruhiwa.
Miezi minane baada ya vita vya Israeli, maeneo makubwa ya Gaza yamegeuka kuwa magofu huku kukiwa na kizuizi cha chakula, maji safi na dawa.
Israeli inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo uamuzi wake wa hivi punde uliiamuru Tel Aviv kusitisha mara moja operesheni yake katika mji wa kusini wa Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni moja walitafuta hifadhi kutokana na vita kabla ya kuvamiwa Mei 6.