Raia wa Uturuki na familia zao waliohamishwa kutoka Gaza kutokana na mashambulizi yanayoendelea Israel wamewasili Istanbul kupitia Misri.
Ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki iliyokuwa na raia 130 wa Uturuki ambao Jumapili usiku walikuwa wamevuka mpaka na kuingia Misri kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Istanbul mapema Jumanne baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo.
Wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na maafisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti Maafa na Dharura ya Uturuki (AFAD) waliwakaribisha katika uwanja wa ndege.
Akiungana na mkewe Sara baada ya miezi miwili, Faisal Said aliwashukuru viongozi hao. Babake Said Rasit Said alimshukuru Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa juhudi zake.
Wakati huo huo, mpiga picha wa Shirika la Anadolu, Mohamed Alaloul, ambaye alipoteza watoto wake wanne na ndugu zake watatu katika shambulio la anga la Israel huko Gaza iliyozingirwa, alifika Istanbul pamoja na mke wake aliyejeruhiwa na mtoto aliyenusurika.
Familia zilizonusurika za waandishi wa habari wanaofanya kazi katika ofisi ya Gaza ya Shirika la Anadolu pia walikuwa miongoni mwa kundi lililokuja Istanbul.
Israel ilianza tena mashambulizi yake ya kijeshi kwenye eneo lililozingirwa siku ya Ijumaa baada ya kumalizika kwa mapumziko ya wiki moja ya kibinadamu na kundi la muqawama la Palestina Hamas.
Takriban Wapalestina 15,899 wameuawa na wengine zaidi ya 42,000 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga na ardhini kwenye eneo hilo tangu Oktoba 7 kufuatia shambulio la kuvuka mpaka la Hamas.
Idadi ya vifo vya Israel imefikia 1,200, kulingana na takwimu rasmi.