Katika ziara yake mjini Uturuki katika wakati huu muhimu, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alihutubia Bunge la Uturuki katika kikao kisicho cha kawaida, ambacho kiliitishwa kuonyesha uungaji mkono kwa kadhia ya Palestina.
Akiangazia mashambulizi ya Israeli dhidi ya ardhi za Palestina hususan Gaza, Abbas siku ya Alkhamisi alisisitiza kuwa "Wapalestina wanasimama dhidi ya 'Vuguvugu la Kizayuni' linalotaka kudhibiti eneo zima."
Abbas pia alisema kwamba Palestina "inathamini sana" msimamo mkali wa Uturuki wa kukataa na kulaani "vita vya mauaji ya kimbari ya Israeli dhidi ya Wapalestina."
"Tunawaomba wote kusimama pamoja nasi katika kuwakomboa zaidi ya wafungwa 10,000 wa Kipalestina katika jela za Israeli," aliongeza, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kwa ajili ya usitishaji wa mapigano mara moja na wa kudumu.
"Gaza, Jerusalem Mashariki, na Ukingo wa Magharibi ni sehemu moja ya kijiografia ambayo inaunda taifa huru la Palestina kwa mujibu wa sheria za kimataifa," Abbas alisisitiza zaidi na kuongeza kuwa yeye, pamoja na viongozi wote wa Palestina, wameamua kwenda Gaza.
Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari
Israeli inakabiliwa na shutuma za kimataifa kwa kukiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Jeshi la Israeli limewaua zaidi ya Wapalestina 40,000 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na mamlaka ya afya ya Palestina.
Zaidi ya miezi kumi baada ya vita vya Israeli, maeneo makubwa ya Gaza yamebaki magofu huku kukiwa na kizuizi cha kuingiza chakula, maji safi na dawa.
Israeli inashutumiwa kwa mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo katika uamuzi wake wa hivi punde uliiamuru Tel Aviv kusitisha mara moja mashambulizi yake katika mji wa kusini wa Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni 1 walikuwa wametafuta hifadhi.